📌RHODA SIMBA
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka viongozi wa dini nchini kuendelea kuliweka Taifa katika mikono salama ya mwenyezi Mungu na wasikubali kuyumbishwa na mtu yeyote asiyelitakia mema Taifa.
Ameyasema hayo leo Agosti 15 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa jengo la kitega uchumi (Safina house) ambapo amesema Serikali imefurahishwa na kukamilika kwa mradi huo kwa kuwa utachangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Serikali inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na taasisi pamoja na mashirika ya kidini nchini, mbali na kutoa huduma za kiroho, taasisi hizi zinasaidia Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi,
Amesema Kanisa limekuwa likiwajali watoto wenye mahitaji mbalimbali, wajane na masikini wasiojiweza, na kwamba huo ndio utumishi mwema na wito mkuu wa kanisa, huku akilipongeza kanisa Anglikana kwa kazi hizo.
Pamoja na kazi kubwa mnayoifanya, nawahimiza kazi ya kulinda maadili na kukemea maovu, kuwafundisha vijana pamoja na watu wazima wale ambao wanalitumia kanisa kufanya mambo ya hovyo
Dkt.Samia.
Kadhalika amesema kuwa Serikali itaendelea kutambua na kuenzi mchango wa Kanisa Anglikana Tanzania pamoja na kudumisha ushirikiano wa karibu na kanisa hili pamoja na taasisi zote za kidini nchini kwani tukifanya kazi kwa pamoja tutaweza kuongeza kasi ya maendeleo kwa Taifa letu.
Kwa upande wake Askofu Mkuu Kanisa la Anglikana Tanzania, Mha. Dkt. Maimbo Mndolwa amesema kuwa Kanisa halifanyi kazi za injili pekee bali linafanya na kazi za maendeleo na za kijamii.
Hayo yote tunayafanya tukijua ya kwamba mkono wa Mungu unagusa watu kwa njia nyingi na moja ya sababu ya kufanya haya ni kugusa maisha ya watu wenye uhitaji mkubwa
Nawatia moyo Maaskofu kuwa kazi mnayofanya pamoja na maumivu na maneno mengi, Mungu anaona, pasipo na kusemwa hakuna kufanya kazi na palipo na kazi yenye nguvu lazima maneno yatainuka na siku zote ushindi utainuka pale tunaposimama na Mungu,"alisema.
Kadhalika amesema kuwa Ujenzi wa jengo hili la kitega uchumi ulianza mwaka 2017, hadi kukamilika kwa jengo hili, tumetumia shilingi bilioni 8 ambapo katika hizo, shilingi bilioni mbili ni msaada kutoka kwa marafiki zetu wa Trinity Church Wallstreet Newyork, shilingi bilioni tatu ni fedha zetu za ndani na bilioni tatu ni mkopo kutoka benki.
Jengo hili tayari lina wapangaji wa kuaminika na litaliingiza Dayosisi takriban shilingi bilioni moja kwa mwaka, kwa kutumia mapato haya na jitihada zetu za ndani ni dhahiri kwamba mkopo huu tutaulipa kwa kipindi kifupi
Tunataka jengo hili lilete taswira ya kanisa kuendelea kujikomboa kiuchumi na hatimaye liweze kujitegemea kwani kwa muda mrefu kanisa limeendelea kutegemea misaada wakati nchi yetu ina fursa nyingi na rasilimali za kutosha,"amesema.
Nae Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Dkt. Chilongani Dickson amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kujumuika na kuthibitisha kwamba anawajali na kuwatumikia watanzania wa dini zote, makabila na itikadi zote.
Nakupongeza Rais Samia kwa uongozi wako mahiri na kwa kazi nzuri unayoendelea kuifanya wewe na Serikali yako katika Awamu ya Sita kwa maendeleo ya nchi yetu na kwa ustawi wa wananchi wote, tangu umepokea kijiti cha uongozi wa Taifa letu, hujayumba wala kutetereka
0 Comments