BODI ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) imewahakikishia wakazi wa jiji la Dodoma ifikapo mwezi Septemba hali ya upatikanaji wa maji itabadilika baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji unaondelea eneo la Nzuguni wa ujenzi wa tanki la kukusanyia maji lenye ukubwa wa lita laki tano.
Aidha baada ya kukamilika kwa mradi huo zaidi ya lita za maji milioni 7.8 zitazalishwa kwa siku, hivyo kuongeza asilimia 11 za upatikanaji maji katika jiji la Dodoma na kuwanufaisha wakazi 75,968 kutoka eneo la Nzuguni, na maeneo jirani.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa bodi hiyo balozi Joab Masima baada ya kutembelea kujionea maendeleo ya mradi huo ambapo amesema mradi ni mkubwa na utaenda kubadilisha sura ya upatikanaji maji Dodoma licha ya kuwepo kwa vyanzo vingine vya maji kama vile chanzo cha Mzakwe.
Kazi ya uchimbaji na kusambaza mabomba imekamilika na kazi ya kujenga vitako vya matenki vinaenda vizuri nyie mliopo Dodoma tukutane mwezi wa tisa kufungua mradi huu
Balozi Masima
Nae Mkurugenzi
Mtendaji wa DUWASA mhandisi Aron Joseph amesema mradi huo umefikia
asilimia 79 ya utekelezaji wake na lita za maji milioni 7.8 zitazalishwa
kila siku na utapunguza uhaba wa maji kwa asilimia 11 .7
Lengo letu ni kuhudumia wananchi wa Nzuguni na maji yatakayobaki yataenda upande wa pili na kama mnavyoona kazi inaendelea ili ndani ya mwezi wa nane kama unavyosema mkataba wetu tuwe tumekamilisha
Mhandisi Aron
Nae Mstahiki Meya wa jiji la Dodoma Profesa Davis Mwamfupe ametoa rai kwa jamii kutumia vizuri maji yaliyopo ili na wengine ambao hawafikiwi na huduma hiyo waweze kufikiwa.
Hata hivyo ikumbukwe kuwa mradi wa Maji Nzuguni utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 4.8 hadi kukamilika kwake mwezi Agosti mwaka huu.
0 Comments