MAMLAKA ya Mawasiliano Tanzania TCRA imesema kuwa Utoaji wa huduma za mawasiliano ni wa ushindani hivyo umesababisha kuongezeka kwa idadi ya mitandao, matumizi ya TEHAMA na aina za huduma zinazotolewa kwa Wananchi, Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Hayo yameelezwa jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa TCRA Dkt. Jabir Bakari wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA na maendeleo ya Mawasiliano.
Kuenea kwa huduma hizi kunawezeshwa na uwepo wa Sera imara, sheria nzuri na mifumo wezeshi ya kiusimamizi na utoaji leseni, TCRA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia malengo yaliyoainishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa (FYDP III) kwenye sekta ya mawasiliano.
Amesema utekelezaji wake unahusisha mchango wa TCRA kwenye uchumi. Kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa lengo la kuboresha uchumi wa kidijiti na uchumi wa buluu, Kuendelea kuweka mazingira bora ya ushindani kwenye sekta ya mawasiliano ili wananchi wengi waweze kumudu gharama za huduma za mawasiliano
Bakari amesema kuwa TCRA imeweza klinda watumiaji wa huduma za mawasiliano dhidi ya uhalifu mtandaoni kwa kutumia mifumo ya kiusimamizi na kugawa rasilimali za mawasiliano, ikiwa ni pamoja na masafa na kutoa leseni kwa watoa huduma zinazowezesha kuongeza idadi ya watumiaji wa intaneti ili kufikia lengo la asilimia 80 ifikapo 2025.
Aidha amesema kuwa Ufuatiliaji na Utekelezaji katika kipindi cha kuanzia Julai 2022 mpaka Juni 2023, TCRA imeendelea kuwasimamia watoa huduma za mawasiliano kwa kuhakikisha wanatoa huduma kwa mujibu wa masharti ya leseni zao pamoja na kuzingatia viwango vya ubora ambavyo vimewekwa kwenye kanuni na sheria zinazoongoza sekta ya mawasiliano nchini.
Amesema maboresho makubwa ya mifumo ya udhibiti wa Sekta ambapo kwa sasa tumejenga uwezo wa kufuatilia ubora wa huduma tukiwa ofisini, ili kuhahikisha watoa huduma za mawasiliano ya simu na intaneti, utangazaji (Radio na Televisheni) na posta wanatoa huduma kwa ufanisi na kwa kuzingatia ubora.
TCRA ilianzishwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Namba 12 ya mwaka 2003 baada ya kuunganishwa kwa iliyokuwa Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC) na Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC). TCRA ilianza kutekeleza majukumu yake tarehe 1 Novemba 2003, Kazi na Majukumu ya TCRA kwa mujibu wa Kifungu Na. 5 cha Sheria wajibu wake ukiwa ni Kuhimiza ushindani bora na uchumi wenye tija, Kulinda haki na maslahi ya watumiaji, Kuhamasisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa watumiaji wote ukijumuisha watumiaji wenye kipato kidogo, walioko vijijini na watumiaji ambao wako katika maeneo yasiyokuwa na mvuto wa kibiashara.
0 Comments