THBUB YAIOMBA SERIKALI NA WADAU KUANDAA PROGRAMU MAALUMU ZA KUWASAIDIA WANAWAKE.

📌RHODA SIMBA

TUME ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeiomba Serikali na wadau mbalimbali kuandaa programu maalum za kuwasaidia wanawake hasa wa vijijini kutumia teknolojia katika kujikwamua kiuchumi na kuendana na kasi ya usawa wa kijinsia.

Hayo yamesemwa na  Mwenyekiti wa Tume hiyo  Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tamko la Tume hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Mwanamke  ambapo  ametoa wito kwa kwa wanawake kuendelea kujiamini na kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

"Siku hii muhimu pia inatukumbusha jukumu walilonalo wanawake wa kiafrika ambao ni uti wa mgongo wa uchumi wa ndani kama wakulima, wajasiriamali, wafanyabiashara, wanasayansi, na viongozi katika sekta nyingine nyingi,

Katika kuadhimisha siku hii muhimu, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora inaungana na jamii na wadau mbalimbali katika kutambua mchango wa wanawake wa Afrika ambao walipigania kwa dhati ukombozi na maendeleo ya bara hili 

Jaji Mstaafu Mwaimu

Aidha, Jaji Mstaafu Mwaimu amesema kuwa THBUB inaendelea kuwaenzi waanzilishi wa Umoja wa Wanawake wa Afrika kwa ushujaa wao, ambapo umechangia kuhamasisha haki za wanawake na usawa wa kijinsia katika ajenda ya ukombozi wa Afrika.

Viongozi wanawake, wengi tunaowaona leo kote barani Afrika, wanasimama juu ya mabega ya wanawake hawa jasiri, ambao walijitolea maisha yao kwa maendeleo ya Afrika

Jaji Mstaafu Mwaimu

Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa THBUB inaendelea kutambua na kuthamini jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutoa kipaumbele katika masuala ya kukuza usawa wa kijinsia na kuyaweka kuwa ni miongoni mwa ajenda muhimu za maendeleo za kitaifa na utekelezaji wake katika nyanja mbalimbali.

THBUB inatambua pia kuwa Serikali imeweka msukumo mkubwa katika suala la kuhusisha masuala ya kijinsia katika sera, mikakati, programu za kisekta na kitaifa; uwezeshaji wanawake na kuzuia na kutokomeza ukatili wa kijinsia

Jaji Mstaafu Mwaimu

Tarehe 31 Julai ya kila mwaka ni maadhimisho ya Siku ya Mwanawake wa Afrika. Mwaka 1962 Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Barani Afrika iliazimia kuadhimisha siku hii kwa lengo la kuhamasisha usawa wa kijinsia, uwezeshaji wa wanawake, na kutambua mchango wao mkubwa katika ukombozi na maendeleo ya Bara la Afrika.

 

Post a Comment

0 Comments