MATOKEO YA KIDATO CHA SITA MSALATO SEKONDARI YAMKOSHA MHE. SENYAMULE

 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU

MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule ameipongeza Shule ya vipaji maalumu ya Sekondari ya Wasichana ya Msalato Mkoani Dodoma kufuatia matokeo mazuri ya kidato cha Sita kwa kupata ufaulu wa alama ya daraja la kwanza 139  na 6 kwa daraja la pili.

Pongezi hizo amezitoa  leo tarehe 17,7.2023 wakati ya ziara yake ya kikazi ya kukagua  hatua ya ujenzi wa mabweni manne, vyumba saba vya madarasa na matundu 10 ya vyoo katika shule hiyo na Shule ya Sekondari Bihawana ambapo ujenzi wa matundu sita ya vyoo, bweni moja na vyumba vinne vya madarasa chini ya fedha kutoka serikali kuu. Katika shule ya Sekondari Msalato awamu ya kwanza ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 428 na awamu ya pili shilingi milioni 260 ikiwa ni nyongeza kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopangwa kuhitajika mabweni mawili ya ziada na Sekondari ya Bihawana shilingi milioni 227.2

Nichukue nafasi hii kuwapongeza walimu na wanafunzi kwa kuufaharisha Mkoa wetu wa Dodoma, tunatamani kila mtu anayefanya kazi Mkoani hapa aifaharishe kwa nafasi yake kama hivi mlivyofanya ninyi hongereni sana mmetupa heshima kubwa sana na ni mategemeo yetu kuwa mtaendelea kufanya vizuri zaidi

Mhe.Senyamule 

Awali, Mhe.Senyamule amekagua ujenzi unaoendelea shuleni hapo na kuwaasa wakandarasi wanaosimamia miradi kuhakikisha wanaongeza kasi ya umaliziaji wa miradi hiyo kwa viwango vinavyotakiwa kwa kuzingatia muda uliobaki ili wanafunzi wa kidato cha tano wanapoingia waweze kutumia miundombinu hiyo, ikiwa imekamilika kwa ubora unaotakiwa.

Lazima siku zilizobaki mjitahidi kuongeza kasi na kuongeza ubunifu  ili kuendana na wakati  uliobaki kwa kuzingatia ubora unaotakiwa, ongezeni idadi ya mafundi na ongezeni masaa ya kufanya kazi, hapa inahitajika speed and accuracy bahati nzuri hapa umeme upo tumieni nafasi hii kukamilisha kazi hii

Mhe.Senyamule

Akiwa katika Shule ya Sekondari ya Bihawana Mkuu wa Shule hiyo Mwalimu Liberatus Nkilema amesema ujenzi katika Shule hiyo uko katika hatua za ukamilishaji na mkakati uliopo ni kukamilisha mradi huo wa ujenzi ifikapo tarehe 30/07/2023.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri amesisitiza umakini katika hatua ya umaliziaji wa mradi ili kuwa na majengo bora yatakayodumu kwa muda mrefu. Shekimweri pia amesema Mkoa wa Dodoma umefanya vizuri sana katika matokeo ya kidato cha sita ambapo katika Shule kumi bora kitaifa, Dodoma ziko shule 5 na katika Wilaya ziko Shule 10.

Naye Mwanafunzi Gloria Frank Shirima Dada Mkuu wa Shule ya Sekondari Msalato akiongea kwa niaba ya wanafunzi wenzake  amemshukuru Mhe, Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa  Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuboresha sekta mbalimbali hususani sekta ya elimu ameahidi kuongeza bidii kwenye masomo ili kuongeza ufaulu wa shule na kutendea haki bidii za Mhe. Rais.

Bihawana na Msalato ni miongoni mwa Shule za Sekondari nchini zilizopokea fedha kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha Tano wanaotaraijiwa kuripoti kuanzia tarehe 14 Agosti 2023. Bihawana Sekondari  ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 227.2 kwa ajili ya ujenzi wa matundu 6 ya vyoo, ujenzi wa Bweni 1 na vitanda 40, vyumba vinne vya madarasa vikiwa na jumla ya viti na meza 160.

 


Post a Comment

0 Comments