WAZIRI wa Nchi
Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Angellah Kairuki
ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu kuhakikisha Walimu waliostahili kupandishwa
vyeo, hata wale ambao hawakupanda kwasababu mbalimbali na kuendelea kukaa katika
cheo kimoja kwa muda mrefu taarifa zao ziwasilishwe katika mamlaka husika.
Kairuki ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua Mafunzo wa uelewa wa pamoja kuhusiana na mfumo wa taarifa za watumishi kwa maafisa wa tume ya Utumishi wa Walimu.
Amesema ni vema mkahakikisha madai mbalimbali ya malimbikizo ya mishahara ya Walimu yanaingizwa Katika mfumo wa kiutumishi na orodha iwasilishwe Katika Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Pia ameitaka Tume ya Utumishi wa Walimu kuhakikisha inafuatilia madai ya Walimu ya likizo pamoja na uhamisho ili Walimu waweze kupata malipo yao kwa wakati.
Kairuki ameongeza kuwa Tume ya Utumishi wa Walimu kuendelea kuondoa changamoto zote na kuona umuhimu wa kuendelea kuwa karibu na Walimu na kutumia lugha zenye staha.
Kwa upande wake katibu Tume ya Utumishi wa Walimu Paulina Mkwama amesema kuwa katika kutekeleza majukumu yao kuna changamoto mbalimbali ambazo zimejitokeza hususani kwa wale ambao wanawahudumia ambao ni Walimu na kusababisha malalamiko.
Amesema kuwa malalamiko hayo ni pamoja na upandishaji wa madaraja, unatokana na ombwe kubwa ambalo lipo baina ya watumishi wa Tume ya Utumishi wa Walimu wilayani pamoja maafisa Utumishi ambao wanafanya kazi katika mfumo.
0 Comments