MWENYEKITI wa Bodi ya kahawa Prof. Aurelia Kamuzora amewaomba wakulima wa mikoa inayolima zao la Kahawa kukubali makato ya Sh.213 kwa kilo kwa ajili ya kuchangia Mfuko wa uendelezaji Kahawa na kuchochea uzalishaji wake.
Ombi hilo amelitoa leo jijini Dodoma kwenye mkutano wa 13 wa wadau wa Kahawa nchini amesema kupitia fedha hizo Bodi inarudisha maendeleo kwa wakulima ikiwamo kupeleka miche na kusaidia huduma za ugani.
Amesema Mkoa wa Kagera wamekubali makato na kuwaomba Wakuu wa Mikoa, Wilaya na Wabunge kusaidia kuhamasisha wakulima wa maeneo yao kukubali.
Niwahakikishie wakulima mchanganuo wa fedha hii ya makato tumeweka wazi na hakuna fedha itakayopotea, tuna mikakati mingi ya kuhakikisha Kahawa ya Tanzania inaendelea kusifika kwa ubora wake
Profesa Kamuzora
Aidha amesema mafanikio yaliyopatikana kutokana na mikakati ya bodi ya kukwamua zao hilo ni pamoja na kuiingizia nchi fedha za kigeni ambapo kwa msimu uliopita zao hilo liliingiza zaidi ya Dola za Marekani milioni 200.
Amewaomba wakulima kuendelea kulima zao hilo kwa kuwa ni mali na Bodi itahakikisha inatumia makato hayo kutafuta miche ili wapande zaidi.
Tangu uhuru kahawa haijawahi kuzalishwa kwa wingi kama mwaka huu ambapo uzalishaji umefikia tani 82,000 na mikakati iliyopo ni kufikia tani 300,000 kwa miaka ijayo.amesema
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa shirika la CAFE Afrika Samora Mnyaonga amesema wamekuwa wakifanya kazi na wakulima wadogo wadogo wa Kahawa nchini ambapo kwa sasa wanatekeleza Mradi wa kukufua zao la Kahawa katika Mkoa wa Kagera hasa katika zao la kahawa aina ya Robusta.
Amesema Mradi huo unafadhiliwa na kampuni ya JDE ya Uholanzi na Wanatekekeza katika Halmashauri 8 ambapo wamewahamasisha wakulima na miche takribani zaidi ya 600000 imezalishwa .
Hata baada ya kuzalisha Miche hiyo lakini bado hatoshelezi mahitaji kwani wakulima wamehamasika kulima na kuhitaji Miche kwa wingi ambapo bodi ya kahawa na taasisi ya utafiti ya kahawa tumeendelea kushirikiana nao
Amesema jukumu lao kubwa wamekuwa wakihamasisha wakulima, kulima Miche kwa wingi lakini bado kuna changamoto ya Miche kuhitajika kubwa kwani wakulima wameona faida ya kilimo cha zao hilo .
Hata hivyo amesema katika utekekezaji wa Mradi huo wamekutana na changamoto ikiwemo upatikanaji wa pembejeo za kilimo hasa katika maeneo wanayolima zao la Kahawa kwani hakuna wasambazaji.
Hivyo taasisi na makampuni wamefikia wakulima na kuwapa Miche ya kahawa bila kusahau kutoa elimu ili waweze kupata tija ya kilimo chao.
Sambamba na hilo Mtendaji mkuu huyo amesema mikakati yao wamejiwekea hadi kufikia 2024 ambapo Mradi huo ndio unaishia wamejipanga na Sekretarieti ya Mkoa wa Kagera na Halmashauri zake zote na wadau wote kuunganisha nguvu na namna gani baada ya kumalizika kwa Mradi waweze kuendeleza kuzalisha miche kwa mafunzo na mbinu bora bila kusahau masoko ya ndani na nje ya nchi
Mratibu wa Mradi wa kuboresha na kuendeleza zao la kahawa kwa wakulima wadogo wa nyanda za juu kusini kutoka Shirika la Viagroforestry, Rashid Malya, amesema shirika hilo linatekeleza mradi wa CODE-P wa miaka minne ulianza mwaka 2020 na utahitimishwa Mei 2024 ambao unalenga kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi katika mnyororo wa thamani wa zao hilo na kuongeza ajira na kuboresha usalama wa chakula na lishe kwa wakulima wadogo.
Lengo la mradi huu ni kufikia wakulima 24,000 katika wilaya sita za mikoa mitatu ya Mbeya, Songwe na Ruvuma ambapo hadi sasa waliofikiwa ni 21,000 huku wanaume wakitajwa kujishughulisha zaidi katika uzalishaji kuliko wanawake
Malya
0 Comments