KATIBU Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Marry Makondo amesema kuwa dunia kwa sasa imehamia kwenye dijitali hivyo ni lazima Mawakili wa Serikali wageukie huko kwa kutumia teknolijia na akili bandia kutatua migogoro na kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani.
Kauli hiyo ameiitoa Jijini Dodoma wakati akifunga mafunzo ya siku tatu kwa Mawakili wa Serikali yaliyokwenda sambamba na Maadhimisho ya miaka Mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali yaliyokuwa na kauli mbiu isemayo "Miaka mitano ya Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali Tulipotoka, Tulipo na Tunapokwenda"
Kwa sasa dunia imegeukia kwenye teknolojia ambapo Dijitali ndio inaongoza dunia hivyo ni wajibu kwa Mawakili kuelekea huku ili kurahisisha kazi na kutatua migogoro kwa wakati.
Aidha amezishukuru taasisi zote zilizowaruhusu Mawakili wa Serikali kuja kushiriki Mafunzo hayo ambayo yamelenga kuwanoa ili waweze kuongeza ufanisi katika majukumu yao ya kila siku.
Hata hivyo amewataka Mawakili hao wa Serikali kutatua migogoro kwa njia ya majadiliano na Usuluhishi ili kutengeneza Mazingira mazuri yatakayowavutia wawekezaji kuja kuwekeza Nchini.
Nchi ikiwa na migogoro, kesi na matukio yasiyofaa hakuna maendeleo hivyo serikali inatambua kazi kubwa mnayoifanya ila kaongezeni kasi ya utatuzi wa migogoro ili kuwavutia wawekezaji
Kwa upande wake Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Boniphace Luhende ameishukuru Wizara ya katiba na Sheria kwa kushirikiana bega kwa bega na Ofisi ya Wakali Mkuu wa Serikali na wadau wengine kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika.
Dkt, Luhende amesema anaamini baada ya mawakili hao kunolewa kwa siku hizo tatu katika maeneo tofauti tofauti ikiwemo utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na majadiliano itakwenda kupunguza mrundikano wa kesi mahakamani kwani utatuzi utafanyika kwa haraka kwa kuzingatia haki kwa pande zote mbili.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa Serikali, Bi. Sarah Mwaipopo amesema Washiriki walikuwa 600 tangu Jumatatu na wameweza kupitishwa katika maeneo mbalimbali ambayo naamini yatawasaidia katika kazi zao.
0 Comments