ELIMU YA KUZUIA RUSHWA YAWAFIKIA WAFUNGWA DODOMA

 

📌MWANDISHI WETU

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Utumishi wa Umma, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Dodoma imewataka wafungwa wa gereza la Msalato kuwa mstari wa mbele kufichua vitendo vya rushwa vinavyojitokeza kwenye maeneo yao.

Haya yameelezwa Juni 21, 2023 na Afisa TAKUKURU Faustine Malecha wakati akitoa elimu ya rushwa kwa wafungwa wa gereza hilo.

Ni wajibu wako wa kutoa taarifa rushwa inapotokea. Una wajibu wa kutoa ushahidi mahakamani pale inapokulazimu kufanya hivyo. Kutoa taarifa ya rushwa ni lazima useme. Kila mwananchi anawajibika kutoa taarifa za vitendo vya rushwa popote pale alipo

Malecha.

Aidha, amesema kuna wengine wako gerezani kwa sababu tu walishindwa kutimiza masharti hali iliyopelekea kuendelea kuwepo gerezani.

Kwanza niwaambie dhamana ni bure ili mradi utimize masharti. Watu wanadhani dhamana ni kutoa fedha hapana, dhamana ni haki yako.

Kutokana na changamoto zinazowakabili wafungwa gerezani, Malecha ameishauri Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuwa na utaratibu wa kutembelea magereza kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Tume ya Haki za Binadamu ina wajibu wa kusikiliza changamoto za wafungwa.

Baadhi ya wafungwa wa gereza hilo, wameeleza kuwa rushwa imesababisha baadhi yao kufikishwa gerezani. Wamesema Serikali isipochukua hatua za haraka kukabiliana na vitendo vya rushwa sehemu za kutoa haki,  itatengeneza taifa la watu wenye chuki na nchi yao.

Kwa upande wa Sabeth Mshana Afisa TAKUKURU amesema, licha ya changamoto wanazopitia wafungwa gerezani  bado wanayo nafasi ya kutoa taarifa za rushwa ili hatua ziweze kuchukuliwa kwa wale watakao kutwa na hatia.

Ni muhimu kutoa taarifa tujue, hii nchi ni yetu wote. Usipokuwa mzalendo unaiua nchi yako. Palipo na rushwa hakuna haki.  Wapo watu wanateseka kwa kutokujua na kupata elimu ya ruswa. Tunatoa elimu ya kuzuia na kupambana na rushwa lengo ni kufikisha ujumbe kwa wananchi.

Sabeth.

Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya 2007,  iliyotungwa kwa shabaha ya kuanzisha na kuipa nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) inalenga kushughulikia kikamilifu makosa ya rushwa na yale yanayofanana nayo hapa nchini.

 

Post a Comment

0 Comments