ASILIMIA 97 YA WANAOJITAMBUA WANA MAAMBUKIZI YA UKIMWI WANATUMIA DAWA

 ðŸ“ŒJASMINE SHAMWEPU

WAZIRI wa Afya Ummy Mwalimu amebainisha kuwa katika kila watu 100 wanaoishi na Virusi vya Ukimwi watu 86 wanajitambua kuwa wanamaambukizi ya UKIMWI ambao ni sawa na 86% huku wanaotumia dawa wakiwa ni 97% kwa Tanzania.

Waziri Ummy ameyasema hayo leo wakati alipotembelea katika Kituo cha Afya MAKOLE akiambatana na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI Angela Kairuki pamoja na ugeni kutoka mfuko wa Rais wa Marekani wa kupambana na Ukimwi US-PEPFAR, Global Fund na UNAIDS Jijini Dodoma.

Tunawashukuru wadau wetu hawa kwa msaada mkubwa waliotupatia ambao umeisadia Tanzania kupatikana kwa mafanikio makubwa ambayo yameweza kupunguza maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) ambapo katika kila watu 100 watu 86 wanajitambua kuwa wanamaambukizi baada ya kupima na kati yao 97% wanatumia dawa

Waziri Ummy

 

Aidha, Waziri Ummy amesema kuwa katika kila watu 100 Tanzania wenye maambukizi ya Virusi vya UKIMWI na wanaojua hali zao ni asilimia 97 ambao wanatumia dawa na wamefanikiwa kufubaza virusi hivyo kwa kujiepusha na maambukizi ya magonjwa mengine na wanaweza wasiwaambukize watu wengine.

Amesema kuwa lengo la Ugeni huo nchini Tanzania umekuja kuangalia utendaji na utekelezaji wa afua mbalimbali za kupambana na Ukimwi, TB na Malaria na kuona uwezekano wa kuongeza nguvu ili kupunguza maambukizi ya magonjwa hayo.

Pia, Waziri Ummy amesema tatizo hili limewakumba sana wanaume hivyo Serikali itaendelea kuchukua mikakati mbalimbali ya kuwashawishi wanaume kupima UKIMWI ili kuweza kutambua hali ya maambukizi ya VVU.

Waziri Ummy amesema eneo la tatu watakalokwenda kulifanyia kazi ni kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto ambapo Dunia inataka iwe asilimia 5 lakini kwa Tanzania ni asilimia 6.5 ya watoto wanaozaliwa na maambukizi.

Hata hivyo Waziri Ummy ametoa wito kwa Watanzania kwenda kupima kujua hali zao lakini kwa ambao wanajua hali zao dawa za UKIMWI zipo na zinatolewa bila malipo na vipimo vya kujipima mwenyewe vipo kwahiyo Watanzania wajitokeze kupima ili tutokomeze UKIMWI ifikapo mwaka 2030.



 

Post a Comment

0 Comments