WABUNGE wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wamepewa Semina na Ofisi ya Hakimiliki nchini (COSOTA), kuhusu majukumu na fursa zilizopo katika ofisi hiyo ikiwemo kulinda hakimiliki za Wabunifu.
Semina hiyo imefanyika Mei 30, 2023 katika ukumbi wa Msekwa Bungeni jijini Dodoma ambapo Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amefungua semina hiyo na kueleza kuwa, semina hiyo ina lengo la kueleza fursa za kibiashara zilizopo katika Hakimiliki pamoja na kuongeza uelewa kuhusu taasisi hiyo.
Sekta ya Ubunifu nchini inakua siku hadi siku, sisi upande wa Serikali tunandelea kuhakikisha Wabunifu wananufaika na kazi zao pamoja na kuwaelemisha kuhusu umuhimu wa kusajili kazi zao katika ofisi yetu ya COSOTA
Mhe. Chana.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa ofisi hiyo, Bi. Doreen Sinare amesema moja ya jukumu la Ofisi yake ni kuhakikisha Wabunifu wananufaika na kazi zao ikiwemo kupata mirabaha kutokana na matumizi mbalimbali ya kazi hizo.
Na amefafanua kuwa mwaka jana Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ilifanyiwa marekebisho ambapo jukumu la kukusanya limeondoka COSOTA na linakwenda kufanywa na Wabunifu wenyewe kupitia kampuni watakazozianzisha.
Akitoa mada katika semina hiyo Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu Shirika la Miliki Bunifu la Kikanda la Afrika (ARIPO) Flora Mpanju alieleza umuhimu wa kusajili Bunifu ARIPO na nchi Wanachama kulipa ada yake, na kufafanua kuwa zipo faida mbalimbali ambazo nchi inapata kupitia bunifu zake na kusaidia kukuza uchumi wa taifa.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Prof. Kitila Mkumbo alisisitiza kuwa Serikali kukamilisha mchakato wa kusaini Itifaki ya Arusha kwani imechukua muda mrefu na jambo hilo ni la msingi kwani litasaidia kuitangaza nchi na kukuza ubunifu katika eneo la kilimo.
Kwa upande wa wadau wa uzalishaji wa maudhui ya Televisheni Mwasiti Badi kutoka Azam Media na Johnson Mshana kutoka DSTV, waliwaomba Wabunge hao kusaidia kukemea vitendo vya wizi wa maudhui sababu kunapoteza mapato ya Serikali na kunadhoofisha uwekezaji uliyofanywa na makampuni hayo.Halikadhalika naye Meneja Mkoa Ziiki Media Camila Owora aliomba elimu ya hakimiliki kutolewa kwa wingi kwa wasanii na kuelewesha kuhusu kuzingatia mikataba kwani hiyo ni changamoto kubwa wanayokutana nayo kwa Wasanii wa Tanzania.
Mafunzo hayo yamedhaminiwa na Azam Media, DSTV, Shirika la Miliki Bunifu la Kikanda la Afrika (ARIPO), BRELA na ZIIKI Media.
0 Comments