UGONJWA WA SHINIKIZO LA JUU LA DAMU UMEONGEZEKA KWA 95.4%

📌RHODA SIMBA

UGONJWA wa shinikizo la juu la damu umeongezeka kutoka wagonjwa 688,901 kwa mwaka 2017 hadi kufikia wagonjwa 1,345,847 kwa mwaka 2021 sawa na ongezeko la 95.4% katika kipindi hicho cha miaka Mitano.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo leo alipotoa tamko kwa Waandishi wa habari katika Ofisi za Wizara Jijini Dodoma ikiwa ni Maadhimisho ya Siku ya Shinikizo la Juu la Damu Duniani. 

Takwimu hizi zinatuonesha kwamba wagonjwa hawa wenye shinikizo la damu wameonekana kuongezeka takribani mara mbili zaidi kwa kipindi cha miaka mitano.

Waziri Ummy

Aidha, Waziri Ummy amesema kwa ujumla magonjwa yasiyoambukizwa yameongezeka kwa 9.4% kwa kipindi cha miaka mitano kutoka mwaka 2017-2021 kwenye vituo vya Afya chini, wagonjwa hawa wameongezeka hadi kufikia wagonjwa 3,440,708 kwa mwaka 2021.

Pia, ameongezea kwa kusema kuwa takwimu zinaonyesha watu 3-4 kati ya 10 wana shinikizo la juu la damu kwa uchunguzi uliofanywa katika jamii kwenye mikoa ya Pwani, Arusha, Geita, Mtwara, Lindi, Zanzibar, Iringa na Dares Salaam.

Kwa upande wa dawa, Waziri Ummy amesema Wizara imeruhusu dawa za kukabili shinikizo la juu la damu katika ngazi ya msingi kwa kuruhusu dawa tatu (3) ambazo ni Losartan, Amlodipine na Hydralazine kutumika katika ngazi ya kituo cha afya na dawa mbili (2) ambazo ni Nifedipine na Frusemide ambazo hutumika katika ngazi ya zahanati.

Mpango wa Serikali kupitia Wizara ya Afya ni kutoa mafunzo ya utoaji wa huduma za magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo huduma za ugonjwa wa shinikizo la damu kwa watoa huduma 2400 kutoka vituo vya Afya vyote 600 katika mikoa yote 26.

Hata hivyo, Waziri Ummy amesema kuna aina mbili za shinikizo la juu la damu ambalo ni shinikizo la juu la damu la asili (primary hypertension) na shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mengine (secondary hypertension).

Kadiri ya asilimia 90-95 za watu wanaathiriwa na Shinikizo la Juu la Damu la Asili yaani wana ugonjwa huu bila kuwa na chanzo cha kisayansi kinachofahamika.

Waziri Ummy

Katika maelezo hayo ameongezea kuwa Shinikizo la juu la damu linalosababishwa na magonjwa mengine hutokana na magonjwa ya figo, mapafu, mfumo wa homoni ambapo huathiri asilimia 5-10 iliyobaki ya watu wenye shinikizo la juu la damu.

Mwisho, Waziri Ummy amewakumbusha Watanzania juu ya umuhimu wa kubadili mtindo wa maisha kwa kuzingatia ufanyaji wa mazoezi, kuepuka tabia bwete, kuepuka matumizi ya tumbaku na bidhaa zake na kupunguza matumizi ya vilevi. 

Pia, tuzingatia ulaji unaofaa wa mlo kamili wenye mboga mboga na matunda ya kutosha ili kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya magonjwa, kupunguza matumizi ya chumvi, sukari na vyakula venye mafuta mengi, pamoja na kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha angalau kiasi cha lita 1.5 ya maji kwa siku.

Ummy Mwalimu

 

Post a Comment

0 Comments