TANZANIA inatarajia kupata miradi ya hifadhi ya mazingira na mabadiliko ya
tabianchi ikiwemo nishati jadidifu yenye thamani ya shilingi trilioni 42.4 kwa
mujibu wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (Nationally Determined Contribution-NDC) itakayosaidia
katika kupunguza ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa.
Fursa hiyo imekuja kutokana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.
Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwakutanisha Marais watano kutoka Zambia, Zimbabwe,
Malawi, Botswana, Makamu wa Rais wa Angola na watendaji kutoka Benki ya Dunia
na Benki ya Maendeleo ya Afrika katika uzinduzi wa mtandao wa uzalishaji wa
pamoja wa nishati jadidifu kwa nchi za kusini mwa Afrika na kujadili fursa za
uwekezaji katika sekta hiyo na miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya
tabianchi.
Hayo yamebainishwa leo Mei 11, 2023 jijini Dodoma na Kaimu Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama wakati akifungua Warsha ya Kujadili
Matokeo ya Mkutano wa 27 na Maandalizi ya Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa
Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Amesema kuwa miradi hiyo itafadhiliwa na Benki ya Dunia, Taasisi ya Afrika
50 na Shirika la Nishati la Afrika kwa kushirikiana na kampuni ya China
Renewable Energies ambapo Kampuni ya Equinor iliahidi kukamilisha
makubaliano ya mkataba wa ufadhili wa mradi wa gesi ifikapo Disemba 08, 2022.
Akiendelea kutaja mafanikio ya mkutano huo, Dkt. Mkama amesema Kampuni ya
TAQA ARABIA ya Misri imeahidi kujenga vituo 12 vya kusambaza gesi asilia
kuanzia mwaka 2023 pamoja na kujenga uwezo wa vijana kuhusu teknolojia ya gesi
katika vyombo vya usafiri.
Mtakumbuka katika Mkutano wa COP 27 Tanzania ilikuwa na banda lake ambalo uwepo wake umetoa fursa kubwa kwa Tanzania kujulikana na kupatikana kirahisi wakati wa mikutano ikiendelea. Hali ambayo iliwezesha kufanya majadiliano na kutoa ufafanuzi kuhusu fursa za uwekezaji na ushirikiano na vipaumbele vya nchi kuhusu hifadhi na usimamizi wa mazingira
Kaimu Katibu Mkuu ameongeza kuwa Shirika la The Nature Conservancy (TNC) lipo tayari kuisaidia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuanza biashara ya kuuza Hatifungani za Bluu (Blue Bond).
Itakumbukwa kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na programu
ya uchumi wa bluu na kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika bara la Afrika
inayofadhiliwa na Benki ya Dunia. Serikali ya Norway imeahidi kuendelea
kuisaidia Tanzania katika masuala ya mabadiliko ya tabianchi, hususan
utekelezaji wa Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC).
Mkutano wa 27
ulifanyika Sharm El Sheikh nchini Misri na Mkutano wa 28 unatarajiwa kufanyika Novemba
30 hadi 12 Disemba 2023 jijini Dubai katika, Muungano wa Falme za Kiarabu.
0 Comments