SERIKALI imesema
inatambua mchango wa sekta binafsi nchini na imeahidi kuendelea kushirikiana
nazo huku ikikiri kwamba haiwezi kufika kila eneo kuwafikia
wananchi hususani katika masuala ya ajira na fursa mbalimbali za
vijana nchini.
Akizungumza leo Mei 11 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa mradi wa kuimarisha sekta binafsi ya Feed the future Tanzania uliopo chini ya shirika la maendeleo la kimataifa la Marekani (USAID) Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Hussein Mohamed amesema kama Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi hasa katika masuala ya ubunifu.
Tunaamini kupitia sekta binafsi tutapata ugunduzi mkubwa kwa kushirikiana na sekta mbalimbali nchini katika kuiletea maendeleo nchi yetu pia katika kueneza matumizi ya sayansi na teknolojia itakuwa rahisi na hili litachangia kukua haraka kwa nchi kwa maana kuzingatia ajenda yetu ya 20/30 kuhakikisha kilimo kinakuwa kwa 10%
Amesema mradi
huo utachangia katika kutekeleza dira ya maendeleo ya 2030, na kuongeza kuwa
Tanzania kwasasa ina takribani vijana milioni 16 na muongo mmoja uliopita
vijana wengi walikuwa wanategemea ajira kutoka serikalini na wizara imeamua
kutengenezea mazingira ya kujiajiri kupitia sekta ya kilimo.
Tumekuwa na programu nyingi za kuhakikisha hili linafanikiwa kwa kufanya vijana wengi kuacha kutegemea ajira za serikali na lengo la wizara ni kuhakikisha kilimo kinawavutia vijana wengi na wao wanaingia kwenye kilimo
Dkt. Mohamed ameongeza kuwa wakifanikiwa kuboresha kilimo na kuwavutia vijana wataweza kuisaidia serikali kwenye utegemezi wa ajira wanapotoka vyuoni.
Naye Mkurugenzi wa misheni ya USAID Kate Somvongsiri amesema USAID imetoa zaidi ya million 12 ili kuimarisha ujasiri wa vijana katika sekta za kilimo Tanzania.
Amesema shughuli ya kuimarisha Sekta binafsi ya Feed the future Tanzania inatoa ruzuku kwa vyama vya wafanyakazi binafsi mashirika, na makampuni makubwa ambayo yataboresha Mazingira wezeshi ya biashara na kupanua fursa za Kiuchumi.
Kwa upande wake Meneja wa Justin Natural Honey Bw. Justin Mgeni mfugaji wa nyuki, amesema kuwa baadaa ya kuhitimu elimu ya chuo Hakuhitaji kusubiria suala la ajira aliamua kujikita katika ufugaji wa Nyuki.Amesema lengo kuu lililomsukuma kufanya hivyo ni baada ya kuona kuna changamoto ya ufungashaji, ukosefu wa kupata bidhaa bora za mazao ya Nyuki na kuamua kuleta vifaa mbalimbali ili kukabiliana na suala hilo.
Pia niliona kuna changamoto ya kupata ajira lakini vijana wengi wanaweza kujikita huko, kwahiyo ilikuwa ni njia pekee ya mimi kukabiliana na changamoto ya ajira baada ya kuhitimu chuo
Ameongeza kuwa kupitia mradi wa Feed the Future utawasaidia kujulikana zaidi na kuifanya shughuli yake kuwa rasmi kutokana na kukosa baadhi ya vitu kutokana na suala la mtaji.
Naye Mkurugenzi wa SANAVITA CO. LTD Jolenta Joseph, Kampuni inayohusika na kukabiliana na Utapiamlo, ameiomba serikali kuhakikisha inaweka wazi kila kitu pale wanapokuwa wanasajili kampuni ikiwemo suala la kulipia kodi ili kuepusha migongano inayoweza kujitokeza wakati shughuli zikiwa zinaendelea.
Tunaishukuru serikali kwa kutuletea mradi wa BBT, kwani umeweza kuwainua vijana wengi kukabiliana na changamoto ya ajira, pia na huu mradi wa Feed the Future utaweza kutufungulia njia ya kujitangaza zaidi ndani na nje ya nchi, na endapo serikali itaendela kuwekeza nguvu kwa vijana naamini malengo ya Ajenda 20/30 tutayafikia
0 Comments