SHIRIKA la
Mawasiliano Tanzania (TTCL) , limepongezwa kwa kuendelea kubuni huduma
zinazochochea maendeleo ya sekta ya Mawasiliano hapa nchini.
Akizungumza Bungeni jijini Dodoma leo Mei 18 mara baada ya kukagua baadhi ya mabanda ya maonesho yaliyoandaliwa kuelekea bajeti ya Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson amesema Shirika hilo limejipambanua katika utoaji wa huduma zake za Mawasiliano ambapo kwa sasa wameweza kufikisha huduma za Mawasiliano katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Dkt.Tulia amesema kuwa TTCL imeifungua nchi kidijitali jambo ambalo limesaidia kuchochea maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
TTCL wameifungua nchi kimawasiliano ukweli huo lazima tuuseme kwanza hili la kupeleka huduma ya Mawasiliano katika Kilele cha Mlima Kilimanjaro ni jambo la kupongezwa kwa nguvu zote kwani sasa kila mmoja anaweza kuwasiliana na ndugu na jamaa wakiwa hata huko huko kileleni haya ni maendeleo
Dkt.Tulia
Dkt.Tulia amezungumzia pia huduma zinazotolewa na Shirika hilo za majumbani ikiwemo huduma ya Fiber Nyumbani kwako na Smart home kuwa zinasaidia kurahisisha Mawasiliano na kusimamia ulinzi na usalama.
Meneja wa Biashara wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Jijini Dodoma Leyla Pongwe, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Shirika hilo, amesema kuwa kasi ya Shirika hilo katika kuleta mapinduzi ya kimawasiliano ni kutaka kuhakikisha agenda ya Serikali inafanikiwa ya kutaka kufikia Uchumi wa Kidijitali ifikapo 2025.
Serikali ina malengo ya kuhakikisha uchumi wa kidigitali unakuwa kwa kasi ifikapo 2025 sasa jukumu letu kama Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL ni kufungua njia kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa
Amesema TTCL imekuja na huduma mpya yenye malengo ya kurahisisha upatikanaji wa huduma ya Mawasiliano na Usalama kwa mtumiaji wa huduma hiyo.
0 Comments