SERIKALI
imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 5.6 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa skimu
ya umwagiliaji katika Kijiji cha Kongogo, Kata ya Babayu, Tarafa ya Mundemu yenye
ukubwa wa hekta 220.
Hayo
yamebainishwa leo na Bw. Raphael Laizer Meneja wa Mradi kutoka Tume ya Taifa ya
Umwagiliaji wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya utekelezaji wa ujenzi wa
bwawa hilo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, katika eneo
la mradi.
Bw.
Laizer amesema ujenzi wa skimu hiyo unaendelea na uko katika hatua za awali chini
ya mkandarasi wa Kampuni ya M/S CRJE (EA) kutoka China.
Akizungumza
na wakazi wa eneo hilo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa skimu hiyo
ya umwagiliaji, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema azma ya
Serikali ni kuhakikisha nchi inakuwa na kilimo cha kisasa kwa kulima mara mbili
mpaka tatu kwa mwaka, kuhamasisha shughuli za uvuvi na mifugo bila kuathiri
mazingira.
Kilimo cha uhakika duniani kote ni kilimo cha umwagiliaji, kilimo kinachowezesha wananchi kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka
Senyamule
Amesema
sababu za Serikali kuajiri maafisa ugani, kununua vitendea kazi ikiwa ni pamoja
na ununuzi wa pikipiki, kuimarisha vitalu vya mbegu zote ni nyenzo za
kuimarisha usalama wa chakula na kuimarisha sekta ya kilimo.
Nae
Bi. Francisca Ntizi amesema kukamilika kwa skimu hiyo ya umwagiliaji itakuwa ni
fursa hususani ya kuimarisha vyanzo mbadala vya mapato ikiwa ni pamoja kujihusisha
na kilimo zaidi ya mara mbili kwa mwaka, uvuvi na kilimo cha mbogamboga.
Ujenzi
huu wa skimu ya umwagiliaji umeanza Aprili 2023 na utakamilika baada ya miezi
18 ambapo pia rambo litajengwa kwa ajili ya kunyweshea mifugo.
0 Comments