📌 MWANDISHI WETU
SERIKALI kupitia Ofisi
ya Makamu wa Rais imezitaka Taasisi
zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi
ya 100 kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2024.
Pia, imezielekeza taasisi zinazoandaa chakula na kulisha watu zaidi ya 300
kwa siku kusitisha matumizi ya kuni na mkaa ifikapo Januari 31, 2025.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo April 12, 2023 jijini
Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dkt.
Selemani Jafo amesema Serikali inazihimiza taasisi hizo kwa sasa kutumia
nishati mbadala ambayo ni safi kwa ajili ya kupikia.
Kwa Mamlaka niliyopewa chini ya Kifungu cha 13 cha Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191, natoa Katazo Kwa Taasisi zote za Umma na Binafsi Tanzania Bara zinazoandaa chakula na kulisha watu kuacha matumizi ya mkaa na kuni
Dkt. Jafo.
Waziri Jafo amesema watumiaji wakubwa wa nishati za kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia ni taasisi za umma na binafsi, hivyo kutokana na athari zake kimazingira, kiafya, kijamii na kiuchumi, Serikali imeandaa Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji wa Dira hiyo kwa kipindi cha miaka kumi hadi kufikia 2033.
Pamoja na urahisi na unafuu wa upatikanaji wa nishati hiyo, matumizi ya kuni na mkaa yanaathiri afya ya mtumiaji kwa kusababisha magonjwa yatokanayo na kuvuta hewa chafu ambayo huathiri mapafu, moyo na matumizi ya muda mrefu wa nishati hiyo pia husababisha magonjwa ya macho
Dkt. Jafo.
Ameongeza kuwa Ripoti ya Tatu ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2019
inaonesha kuwa kasi ya uharibifu wa misitu ni kubwa na kila mwaka zaidi ya
hekta 469,420 huharibiwa kutokana na ukataji wa miti kwa ajili ya matumizi ya
kuni na mkaa.
Waziri Jafo amefafanua kuwa kwa mujibu wa takwimu zilizopo inakadiriwa kuwa
asilimia 16 ya ardhi imeharibika na inakabiliwa na kuenea kwa hali ya jangwa na
ukame kutokana na watu wengi kufanya shughuli zisizo endelevu ikiwemo kutumia
nishati ya kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia kutokana na nishati hiyo
kupatikana kwa urahisi na watu wengi wanaweza kumudu gharama yake.
Akifafanua zaidi Dkt. Jafo amesema kutokana na athari hizo zilizojitokeza,
kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kujenga uchumi wa viwanda, hivyo matumizi
ya nishati mbadala ikiwemo mkaa mbadala yatatoa fursa ya viwanda vya
kutengeneza mkaa mbadala sanjari na kuzalisha majiko sanifu na banifu kwa
ajili ya matumizi fanisi ya nishati hiyo.
Hivyo, ametoa wito kwa makampuni ya gesi, mkaa mbadala na majiko banifu
yatumie katazo hili kama fursa ya uzalishaji wa bidhaa hizo kwa wingi kwa ajili
ya kupanua wigo wa masoko kwa taasisi hizo.
Itakumbukwa kuwa Juni Mosi 2021, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa alitoa tamko la Wiki ya Mazingira Duniani na kuzielekeza
Taasisi, Mashirika ya Serikali na Sekta Binafsi zianze kutumia nishati mbadala
kwa kupikia na shughuli nyingine za uzalishaji.
0 Comments