WCF "MALIPO YA FIDIA YANAONGEZEKA MWAKA HADI MWAKA"

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

IMEELEZWA kuwa Kabla ya kuanzishwa kwa WCF, malipo ya fidia nchini kwa mwaka mzima yalikuwa chini ya shilingi milioni 200 lakini baada ya kuanzishwa kwa WCF malipo yanaongezeka mwaka hadi mwaka.

Hayo yamesemwa leo Machi  2  2023 jijini Dodoma  na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa fidia kwa wafanyakazi WCF Dkt. John Mduma alipokuwa akielezea utekelezaji wa majukumu ya Mfuko huo.

Amesema kuwa Serikali kupitia WCF imeleta mageuzi makubwa nchini, kwa takwimu za mwaka 2016/17, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 538 na kiasi cha shilingi milioni 613.84 kililipwa.

Kwa mwaka 2021/2022 pekee, WCF ililipa fidia kwa wanufaika takribani 1,600 na kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni 9.33 kililipwa, Hadi kufikia tarehe 30 Juni 2022, WCF imelipa mafao yenye thamani ya Shilingi Bilioni 44.61 kwa wanufaika mbalimbali ikiwa ni ongezeko kubwa kwa kulinganisha na kipindi cha kabla ya kuanza kwa WCF ambapo malipo ya fidia yalikuwa chini ya Shilingi Milioni 200 kwa mwaka,"amesema.

Aidha amesema kwa hesabu zisizokaguliwa, katika kipindi cha Julai 2022 hadi Desemba 2022, WCF ililipa mafao ya jumla ya Shilingi Bilioni 6.19 kwa wanufaika 1,004 na hivyo kufanya wanufaika wa Mfuko toka kuanzishwa kwake kufikia 10,454 ambao wamelipwa jumla ya Shilingi Bilioni 49.44.  

Pia amesema WCF ni mdau muhimu katika kupunguza umaskini kwenye Taifa kwa kuwahakikishia kipato wafanyakazi wanaopata ulemavu wa kudumu kutokana na ajali au magonjwa yatokanayo na kazi.

Kabla ya kuanzishwa kwa WCF, wafanyakazi wa sekta binafsi waliopata ulemavu walikuwa wakilipwa kwa mkupuo kiasi cha Shilingi 108,000 tu na wafanyakazi wa sekta ya umma waliopata ulemavu wa kudumu walikuwa wakilipwa kwa mkupuo kiasi cha Shilingi Milioni 12 tu bila kujali kama ulemavu huo umewapotezea kabisa uwezo wa kufanya kazi na kupata kipato

Mfuko umekuwa ukilipa fidia kwa mfumo wa pensheni ya kila mwezi kwa wategemezi au wafanyakazi waliopata ulemavu unaozidi asilimia 30 inayofikia hadi asilimia 70 ya mshahara wa mfanyakazi jambo linalomwezesha mfanyakazi au wategemezi wao kuepukana na umaskini,"amesema.

WCF ni taasisi ya hifadhi ya jamii iliyoanzishwa chini ya kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi [Sura 263] kwa lengo la kulipa fidia kwa wafanyakazi wanaopata ulemavu au kufariki kutokana na magonjwa au ajali zitokanazo na kazi wanazozifanya kwa mujibu wa mikataba yao ya ajira.

 


Post a Comment

0 Comments