UHABA WA MAAFISA UGANI WATAJWA KUKWAMISHA UKUAJI SEKTA YA KILIMO

 ðŸ“ŒJASMINE SHAMWEPU

PAMOJA na jitihada zinazofanywa na serikali kwenye sekta ya kilimo nchini ikiwemo kuongeza bajeti na kuweka ruzuku kwenye mbolea, uhaba wa maafisa ugani imelezwa kuwa bado ni tatizo ambalo linachangia sekta hiyo kutokuwa na tija kwa wakulima.

Aidha, serikali imetakiwa kuwekeza kwenye kilimo ikolojia ambacho kinalinda afya za watu na mazingira na kuachana na kilimo biashara ambacho kimekuwa kikihusisha matumizi makubwa ya kemikali.

Hayo yamebainisha leo kwenye kongamano la huduma za ugani na kilimo ekolojia kwa wanawake Tanzania, lililoandaliwa na Shirika la Action Aid na kujumuisha wakulima kutoka mikoa ya Singida, Morogoro, Dodoma na Songwe.

Janeth Nyamayahasi, mkulima kutoka Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, amesema kuwa uhaba wa maafisa ugani nchini umekuwa kikwazo kwao kushindwa kupata tija kwenye kilimo.

Amesema kutokana uhaba wa maafisa ugani hasa katika maeneo ya vijijini wakulima wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea hali ambayo inawafanya washindwe kujikwamua kiuchumi kupitia sekta hiyo.

Kwa mfano Wilaya ya Chamino ina vijiji 117 lakini maafisa ugani waliopo ni 50 na hawa wapo katika maeneo ya kata hivyo mkulima hawezi kumsubiri Afisa Ugani atoke kijiji kingine aje ampe mbinu za kilimo cha kisasa wakati msimu wa mvua unazidi kwenda

Kadhalika, amesema sera ya kilimo inasema kuwa afisa ugani mmoja anapaswa kuhudumia kijiji kimoja na kuwafikia wakulima 600.

Amesema kero nyingine iliyopo kwenye sekta hiyo nchini ni uhaba wa vitendea kazi ikiwemo vifaa vya kupimia afya udongo.

Mkulima huwezi kulima kila mwaka pasipokujua afya ya udongo wako hivyo vifaa vinahitajika, tunaipongeza serikali kwa kununua vipimo vya afya ya udongo lakini bado havitoshi kwani vipo katika ngazi ya Halmashauri siyo vijijini kwa wakulima wadogo

Naye, Torati Buzika mkulima kutoka Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro, alisema serikali inatakiwa kukipa kipaumbele kilimo ekolojia ambacho hakitumi kemikali.

Kilimo ekolojia ni kilimo ambacho pia hakina gharama kutokana na kutotumia kemikali hivyo hata sisi wakulima wanawake wa hali ya chini tunaweza kukimudu kwani hata serikali ikiweka ruzuku kwenye mbolea bado wapo wakulima wengi ambao hawawezi kumudu kutoa Sh. 70,000 kwa ajili ya mfuko mmoja wa mbolea

Vile vile, amesema kilimo ekolojia kwa kutumia mbegu za asili kina faida nyingi ikiwemo kulinda afya za walaji  pamoja na mazingira tofauti na mbegu za kisasa ambazo zinahitaji matumizi makubwa ya kemikali.

Ofisa programu wa Action Aid, Elias Mtinda amesema lengo la kongamano hilo ni kuwakutanisha wakulima wanawake kutoka mikoa hiyo pamoja na wadau, wizara za kisekta na mashirika ili kuangalia kero ya uhaba wa maafisa ugani na kutambua mbinu za kilimo ekolojia.

Kilimo ekolojia kinamsaidia mkulima kukabilia na mabadailiko ya tabia ya nchi kutokana na matuzi ya mbegu za asili kustahimili ukame na kutoa mavuno mengi tofauti na zile za kisasa lakini pia hakitumii kemikali na madawa ya viwandani ambayo ni hatari kwa afya za watumiaji

 

Post a Comment

0 Comments