📌JASMINE SHAMWEPU
MKURUGENZI Mkuu Mamlaka ya serikali Mtandao (eGA), Mhandisi Benedict Benny Ndomba amewataka wadau wote wa TEHAMA nchini kushiriki kikamilifu kikao kazi cha serikali mtandao.
Aidha amesema wadau hao wanaweza kushiriki katika kikao hicho kwa kufanya usajili kupitia mfumo wa TSMS (https://tsms.ega.go.tz).
Mhandisi Ndomba ametoa rai hiyo Jijini Dodoma katika kikao na waandishi wa habari leo Februari 6,2023.
Kikao kazi hicho kinatarajiwa kufanyika kwa siku mbili kuanzia Februari 8-10 katika ukumbi wa AICC Jijini Arusha huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama.
Amesema lengo la kikao hicho ni kuwakutanisha wadau mbalimbali wa serikali Mtandao ili kujadili juu ya mafanikio, changamoto pamoja na kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza serikali Mtandao nchini pamoja na kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA katika taasisi za umma sambamba na kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Takribani wadau 1000 wa serikali mtandao kutoka mashirika na taasisi za umma wakiwemo maafisa mashuuri, wajumbe wa bodi, wakuu wa vitengo vya TEHAMA, maafisa TEHAMA, maafisa Rasilimali watu, maafisa mipango, maafisa mawasiliano, wahasibu pamoja na watumiaji wote wa mifumo ya TEHAMA serikalini wanatarajia kushiriki
Ndomba.
Aidha ameongeza kuwa kikao hicho kitaongozwa na kauli mbiu isemayo “Mifumo Jumuishi ya TEHAMA kwa utoaji huduma bora kwa Umma ” ikiwa ni kuhamasisha taasisi za umma kutumia mifumo jumuishi inayowasiliana katika utendaji kazi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Mamlaka ya serikali Mtandao (eGA) ndiyo taasisi iliyopewa jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza juhudi za serikali Mtandao pamoja na kuhimiza uzingatiwaji wa sera, Sheria, kanuni, viwango na miongozo ya serikali Mtandao katika taasisi za umma ili kuhakikisha matumizi sahihi na salama ya TEHAMA yanazingatiwa katika taasisi hizo
0 Comments