JAMII imeshauriwa kuacha kukopa mikopo umiza kiholela ijulikanayo kama (KAUSHA DAMU) na baadala yake wachukue fedha hizo kwa matumizi lengwa kwani wanawake wengi wamekuwa wakichukua mikopo na kufanya mambo yasiyoingiza kipato kama vile kulipa ada, ujenzi wa nyumba na kununua mavazi.
Hayo yamesemwa leo Februari 14 jijini Dodoma na Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) Beng'i Issa wakati alipokuwa akieleza utekekezaji wa majukumu ya baraza hilo ambapo amesema linatoa usimamizi wa vikundi vidogo vya fedha pamoja na kuvilea pia kuvipa ushauri wa jinsi gani viweze kuendelea.
Aidha amesema kuwa kutokana na hali hiyo Baraza limeona kunahaja ya wananchi kupatiwa elimu ya fedha ili wasijikute wameingia katika mikopo hiyo umiza (KAUSHADAMU).
Tusikimbilie mikopo ingawa inasaidia sana watu, mtu akisikia sehemu kuna mikopo anaenda anachukua lakini hajui anaenda kufanyia nini ili azalishe aweze kurudisha mkopo huo, hivyo nawaasa kuchukua mikopo na kwenda kufanyia shughuli za kiuchumi
Kuna mikopo mingine ambayo mtu akikopa asubuhi tu jioni anaanza marejesho au kesho yake asubuhi, mikopo ya hivi siyo mizuri na utakuta taasisi nyingine hata hazijasajiliwa ambapo wengi wao mtu akishindwa kurejesha fedha wanaenda kubeba vitanda na vitu vingine
Hata hivyo baraza limekuwa likisimamia kampuni za ndani kupata tenda katika miradi mikubwa na ya kimkakati inayoendelea hapa nchini ambapo jumla ya kampuni 1771 zimepatiwa tenda.
Watanzania zaidi ya 83,000 wamepata ajira katika miradi ya kimkakati hapa nchini
Pamoja na hayo NEEC inasimamia programu za uwezeshaji (Viwanda Scheme) ambapo wafanyabiashara wenye viwanda vidogo na vya kati hukopeshwa.
NEEC hadi sasa imewezesha kuwapatia zaidi ya Shilingi Bilioni 3.5 wafanyabiashara wenye viwanda vya kati na vidogo katika miradi 62 kwenye mikoa 12 nchini
Vilevile amesema kuwa Baraza huandaa Makongamano ya Kitaifa na maonesho ya mifuko na programu za uwezeshaji ili kuongeza na kukuza uwezo kwa walengwa ambayo ni Kongamano la mwaka la Uwezeshaji, Kongamano la Ushiriki wa Wananchi katika Miradi ya Kimkakati, Maonesho ya mifuko na programu za Uwezeshaji
0 Comments