📌MWANDISHI WETU
KLABU cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma (CPC), kimetoa tuzo ya heshima kwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kutokana na dhamira yake ya kuhakikisha uhuru wa vyombo vya habari unaimarika na kuanza kushughulikia vikwazo vinavyoikabili sekta ya habari nchini.
Tuzo hiyo imetolewa katika hafla ya usiku wa waandishi wa habari mkoani Dodoma iliyoandaliwa na CPC kwa udhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi ya Wazo Huru na mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew.
Akitoa maelezo ya tuzo hiyo iliyopokelewa kwa niaba na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule ambaye ni Mlezi wa chama hicho, Mwenyekiti wa kamati ya utoaji tuzo, Nelly Mtema, amesema Rais Samia alipoingia madarakani aliagiza kufunguliwa kwa vyombo vya habari vilivyokuwa vimefungwa na kuanzishwa kwa mchakato wa mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari nchini ya mwaka 2016 iliyokuwa ikilalamikiwa na wadau kwenye baadhi ya vipengele.
Pia katika uongozi wa Rais Samia amefanikisha kubadilishwa kwa viwango vya ada za usajili wa channel za mtandaoni ambapo kwasasa ni Sh.500,000 badala ya Sh.Milioni moja, hatua hii imewezesha waandishi wengi chipukizi kujiajiri kwa kufungua channel hizo.
Kuhusu uchumi wa vyombo vya habari na waandishi wa habari, Mtema amesema kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, imeundwa kamati maalum ya kuchunguza hali ya kiuchumi kwa vyombo vya habari na waandishi wa habari ili kunusuru uchumi wa sekta hiyo.
Aidha, amesema tuzo ya kiongozi bora wa kitaifa kwa mwaka 2022, imetolewa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dkt.Selemani Jafo kutokana na kuwa kiongozi anayezingatia muda katika utekelezaji wa majukumu yake hasa yanayohusisha waandishi wa habari.
Katika hafla hiyo, CPC ilitoa tuzo ya kutambua mchango wa Wizara Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenye tasnia ya habari iliyopokelewa na Naibu Waziri Kundo huku Mkuu wa Mkoa Senyamule akipewa tuzo ya kutambua ushirikiano anaowapa waandishi wa habari wa Dodoma kwenye utekelezaji wa majukumu yao.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikali kutoka TAMISEMI Ntegenjwa Hossea akipokea tuzo ya Afisa Habari bora kwa mwaka 2022. |
Agusta Njoji akipokea tuzo ya Mwandishi bora wa mwaka 2022 kwa mkoa wa Dodoma |
Rasul Kidindi akiwa na tuzo yake ya Mwandishi Chipukizi mkoa wa Dodoma. |
Jackline Kuwanda akipozi baada ya kupokea tuzo yake ya Mwanachama Bora wa Mwaka wa CPC |
Pia, tuzo ya mwandishi bora wa habari Mkoa wa Dodoma kwa mwaka 2022 alishinda Augusta Njoji kutoka gazeti la Nipashe, Afisa Habari bora ilikwenda kwa Nteghejwa Hosea kutoka Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mwanachama bora wa CPC ilikwenda kwa Jackline Victor na tuzo ya Mwandishi Chipukizi ilitolewa kwa Rasul Kidindi.
0 Comments