CPC YAIANGUKIA SERIKALI USAJILI WA MITANDAO YA KIJAMII YA VILABU VYA WAANDISHI WA HABARI



📌MWANDISHI WETU

KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma(CPC), imeiomba serikali kuondoa malipo ya usajili wa mitandao ya kijamii inayomilikiwa na vilabu vya waandishi wa habari kwa kuwa haiendeshwi kibiashara bali inatoa huduma za kuhabarisha jamii.

Mwenyekiti wa CPC, Mussa Yusuph ametoa ombi hilo alipokuwa akisoma risala ya klabu hiyo kwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew kwenye hafla ya usiku wa waandishi wa habari mkoani Dodoma iliyoandaliwa na CPC kwa udhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi ya Wazo Huru.

Aidha, amesema kwa niaba ya vilabu 28 vya waandishi wa habari nchini, wanaomba serikali kutoa msamaha wa malipo ya blog za vilabu nchini kutokana na mitandao hiyo haiendeshwi kibiashara bali inatoa huduma za kuhabarisha umma.

Blog hizi hazifanyi biashara hivyo kwa mara kadhaa tumeshindwa kulipia TCRA hivyo tunaomba zipewe msamaha ili ziendelee kuhabarisha umma

Aidha, amewaomba wadau kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwamo uhaba wa vitendea kazi na ujenzi wa ofisi ili kubeba idadi kubwa ya wanachama.

“Ofisi yetu kwa sasa imekuwa ndogo hivyo kushindwa kukidhi kubeba idadi kubwa ya wanachama kwa wakati mmoja, pia tuna changamoto kubwa ya thamani za ofisi hivyo tunapata changamoto kubwa pindi waandishi wengi wanapohitaji kutumia ofisi kwa wakati mmoja.”



Uhaba wa vitendea kazi kwa wanachama hasa kipindi ambacho Mkoa unakuwa na shughuli nyingi na kubwa kama vikao vya Bunge na mikutano ya kitaifa, vifaa hivyo ni Kamera na Kompyuta

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri Kundo ameahidi kutembelea ofisi za klabu hiyo na kuangalia namna ya kusaidia kutatua changamoto zilizobainishwa.

Nipongeze klabu ya Dodoma kwa hatua hii kubwa ya kuwa na blog, nipongeze pia kwa kuwa na Ofisi napenda niwahakikishie serikali itaendelea kuwa pamoja nanyi hasa ikizingatiwa serikali imehamia Dodoma, Wizara pamoja na wadau tutaendelea kutatua changamoto za sekta ya habari

Hata hivyo, amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuboresha mazingira ya waandishi wa habari na kuweka misingi ya kisheria ili kupata taarifa.

"Katika gharama ya usajili wa blogs Rais aliagizwa zipitiwe upya na zikapitiwa na tutaendelea kufanya mapitio ili kufikia hatua ambayo kweli itasaidia wanahabari,"amesema.

Post a Comment

0 Comments