📌MWANDISHI WETU
WATU 12 wamefariki
dunia na wengine 63 wamejeruhiwa katika ajali ya gari iliyotokea usiku wa
kuamkia leo Alhamisi Februari 9, 2023 Wilayani Kongwa Mkoani Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa
Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kuwa ajali hiyo imehusisha magari mawili na
kusababisha vifo vya watu 12 (wanaume 8, wanawake 4) na Majeruhi 63
(wanaume 40 wanawake 23).
Ajali hiyo
imetokea usiku katika Kata ya Pandambili Kijiji cha Silwa Wilayani Kongwa,
barabara ya Dodoma - Morogoro.
Majeruhi
wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya ya Kongwa na Kituo cha Afya
Gairo. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkoa wa
Morogoro na majeruhi 2 wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.
Ajali hii
imetokea majira ya saa 6 usiku na imehusisha gari aina ya Lori lenye namba za
usajili T 677 DVX na basi la abiri Kampuni ya Frester
lenye namba za usajili T 415 DPP lililokuwa likitokea Bukoba kwenda Dar es
Salaam.
Mkuu wa Operesheni
na Mafunzo wa Jeshi la Polisi Kamishna Awadh Haji ametaja
chanzo cha ajali hiyo kuwa ni mwendo kasi na uzembe wa dereva wa basi kutaka
kulipita gari la mbele bila ya kuchukua tahadhari na kugongana na Lori
lililokuwa limebeba saruji.
Akizungumza na
wakazi wa Pandamili eneo la ajali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary
Senyamule ametoa rai kwa jamii kutii sheria bila shuruti ili kuepuka ajali.
Serikali ilikuwa na nia njema ya kuruhusu vyombo vya usafiri kutembea usiku, lakini sasa baadhi ya madereva wanaanza kutozingatia Sheria za usalama barabarani, tutaendelea kuwachukulia hatua kali
Mhe. Senyamule.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma amewatembelea majeruhi katika Hospitali ya Kongwa na Kituo cha Afya Gairo kutoa pole na kuwatakia uponyaji wa haraka.
0 Comments