WANANCHI WATAKIWA KUISHI KIDIJITALI

 ðŸ“ŒWMJJWM

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), amewataka Wananchi hasa wa Makundi maalum kutumia fursa zinazotolewa na benki za ndani ya nchi ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza wakati alipotembelea benki ya NMB Makao Makuu Jijini Dar es salaam,  24 Januari 2023,  Waziri Gwajima amebaini fursa mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo na  ambazo zimewanufaisha makundi maalumu wakiwemo Wanawake, Wamachinga na Waendesha Bodaboda wanaofikia idadi ya maelfu. 

Waziri Gwajima amesema, amefarijika kuona benki hiyo inafanya jitihada ya kurahisisha huduma za kibenki kwa Makundi Maalumu hasa yanayosimamiwa na Wizara hiyo. 

Nimekuja kujifunza ni kitu gani nitawaambia hawa Makundi Maalum hasa ikizingatiwa kwamba, tuko kwenye utekelezaji wa Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kama ilivyoelekezwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mara tu alipoingia madarakani

Dkt. Gwajima.

Ameongeza pia, moja ya mambo muhimu katika programu hiyo ni jinsi gani utekelezaji wa uwezeshaji wanawake kiuchumi unavyoendelea kwenye sekta mbalimbali ikiwemo mabenki ambapo NMB ni mojawapo ya benki zenye hisa kubwa Serikalini.

Aidha, Dkt. Gwajima ameipongeza NMB kwa kupiga hatua na kufanya vizuri katika maeneo mbalimbali ya uwezeshaji wananchi kiuchumi. Aidha, ameahidi kuendelea na ziara yake kwenye benki zote sambamba na kuelimisha na kuhamasisha jamii itambue fursa hizi na kuchukua hatua za kujiendeleza kiuchumi jambo ambalo pia litachangia kwenye kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto utokanao na migogoro ya kiuchumi. 

Waziri Gwajima anaendelea na ziara hiyo katika benki nyingine nchini kwa lengo la kuangalia fursa za uwezeshaji wananchi kiuchumi hususani Makundi maalum na kuhakikisha kwa nafasi yake anazisemea ambapo ameitambulisha ziara hiyo kama Operesheni *"Zijue Fursa, Imarisha Uchumi Kataa Ukatili, Kazi iendelee".* 

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa benki hiyo Ruth Zaipuna amesema benki hiyo ina fursa nyingi kwa Makundi yote katika Jamii ambazo zikitumiwa kikamilifu, zitawainua wananchi wengi kiuchumi.

Nia ni kuhakikisha watanzania wengi zaidi wanaingia kwenye mfumo rasmi wa kibenki, fursa ni nyingi kwa bodaboda, machinga na watanzania kwa ujumla wanakaribishwa kuzipata ili kuweza kuinuka kiuchumi

Ruth.



 

Post a Comment

0 Comments