MAKAMU WA RAIS AFUNGUA KONGAMANO LA MAASKOFU KUKABILIANA NA BIASHARA HARAMU YA USAFIRISHAJI BINADAMU

 ðŸ“ŒMWANDISHI WETU

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania imejitolea kuzuia na kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu kwa kuhakikisha inatambua na kushughulikia mambo mbalimbali ya kijamii, kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa ambayo yanawafanya watu kuwa hatarini na kuhusika katika biashara hiyo haramu.

Makamu wa Rais amesema hayo leo tarehe 30 Januari 2023 wakati akifungua Kongamano la Mashauriano la Maaskofu, Wachungaji na Viongozi Wakuu wa Kanisa la Anglikana kutoka Tanzania na Mataifa mengine duniani kuhusu kupiga vita Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu, kongamano linalofanyika Ramada Jijini Dar es salaam.

Amesema Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wengine inaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuharakisha ukuaji wa uchumi, kupunguza umaskini, na kuboresha ustawi wa kijamii na kiuchumi wa wananchi ili kuwaepusha na kadhia ya biashara hiyo. Aidha Makamu wa Rais ameongeza kwamba ili kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu,serikali imeendelea kujenga taasisi imara ili kurahisisha upelelezi na uendeshaji wa kesi za kadia hiyo pamoja na kutunga sheria ikiwa ni pamoja na Sheria ya Kupambana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu ya mwaka 2008.

Aidha Makamu wa Rais ameeleza kwamba Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi na Uhamiaji, Mahakimu, Waendesha Mashtaka, Viongozi wa Serikali za Mitaa, Maafisa Ustawi wa Jamii na wadau wengine ili kuwapatia maarifa na zana za kukabiliana na Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu pamoja na kuanzisha Sekretarieti ya Kuzuia biashara hiyo ikiwa ni nchi ya pili barani Afrika kuwa na chombo maalum cha kuzuia na kupamba na na suala hilo.

Makamu wa Rais amesema kutokana na juhudi zilizofanywa naTanzania katika kukabiliana na biashara haramu ya usafirishaji binadamu, Serikali imefanikiwa kuokoa wahanga 905 pamoja na kuwa na jumla ya kesi 73 za usafirishaji haramu wa binadamu zinazowahusisha wahalifu 133 ambao wamefikishwa mahakamani huku jumla ya wahalifu 86 wakikutwa na hatia na kuhukumiwa vifungo gerezani.

Makamu wa Rais ametoa wito kwa Kanisa kutambua jukumu kubwa walilonalo la kuwaelimisha waumini wake kutenda haki ikiwemo kuwalipa vema wafanyakazi wao wanyumbani badala ya kujinufaisha na kuwadhulumu. Pia Dkt. Mpango ametoa wito kwa Kanisa pamoja na mashirika mengine ya kidini nchini kushirikiana na serikali katika kuwatambua wahanga wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu na kuwasaidia kwa kuwapatia makazi, matibabu, huduma za kiroho na pia kutoa ushauri nasaha utakaorahisisha waishi vema katika jamii.Amesema hakuna budi kwasasa Kanisa kushirikiana na Serikali kuwabaini wahusika na kuwaripoti kwenye mamlaka husika ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria ili kulinda vizazi vya sasa na vijavyo.

Akimkaribisha Makamu wa Rais katika Kongamano hilo, Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dkt. Maimbo Mndolwa amesema katika mazingira mbalimbali waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu wanaingia katika kadhia hiyo pasipo kutambua na baadae wanawekewa mazingira ya kukubaliana na hali hiyo ya unyonyaji na uondoaji utu. Amesema suala hilo ni dhambi kubwa katika dunia ya sasa hivyo kama kanisa wamekusanyika kutafuta njia mbalimbali za namna ya kumaliza tatizo hilo.

Askofu Mndolwa amesemaTanzania imechaguliwa kuwa Mwenyeji wa Mkutano huo kutokana na jitihada zinazofanywa na serikali kupamba na biashara hiyo ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Awali Katibu Mkuu wa Taasisi ya Mashirikiano ya Maendeleo ya Kanisa la Anglikana Duniani (USPG) Mchungaji Dkt. Duncan Dormor kutoka nchini Uingereza amesema katika Kongamano hilo wanatarajia kubadilishana uzoefu pamoja na kuweka nia thabiti ya kufanya kazi pamoja ulimwenguni ya kupiga vita biasharaharamu ya binadamu kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine. Ameongeza kwamba unyonyaji na utoaji haki na utu wa mwanadamu kupitia biashara haramu ya binadamu unakiuka Imani ya kikristo inayoeleza kila binadamu ameumbwa kwa mfano wa Mungu na ana thamani kubwa mbele yake.

Kongamano Mashauriano la Maaskofu Wakuu, Maaskofu na Viongozi wa Kanisala Anglikana Duniani kuhusu kupiga vita Biashara Haramu ya Usafirishaji Binadamu linafanyika kwa siku saba likiwa na kauli mbiu isemayo“Set my People Free: The Call of the Church against Human Trafficking.”



 

Post a Comment

0 Comments