DKT. JAFO AMTAKIA HERI YA KUZALIWA MHE. RAIS SAMIA KWA KUPANDA MITI DODOMA

 

📌MWANDISHI WETU

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira)Mhe. Dkt. Selemani Jafo amesema ndani ya kipindi cha miaka miwili Tanzania imepiga hatua katika kusukuma mbele ajenda ya mazingira. 

Amesema hayo leo Januari 27, 2023 wakati akizungumza baada ya kuongoza zoezi la upandaji miti katika kituo cha kulea watoto cha Nyumba ya Matumaini kilichopo Miyuji jijini Dodoma kumtakia heri ya kumbukizi ya siku ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia, amempongeza RaisDkt. Samia kwa kuwa mwanamazingira namba moja nchini na duniani akimtaja kuwa amekuwa akihamasisha wananchi kushiriki shughuli za kuhifadhi mazingira katika maeneo mbalimbali.

Amesema Desemba 21, 2017 alizindua Kampeni ya Kukijanisha Dodoma katika eneo la Mzakwe jijini Dodoma hivyo katika kumuenzi mabalozi wa mazingira wamefanya kazi nzuri ya kuhamasisha upandaji miti.

Dkt. Jafo pia amewashukuru mabalozi wa mazingira na wataalamu kutoka Jiji la Dodoma kwa kuandaa zoezi hilo na kusema kuwa ni la muhimu katika kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

Waziri Jafo amesema kuwa zoezi la upandaji miti limekuwa na mwitikio mkubwa miongoni mwa wanafunzi wa shule, vyuo na jamii kwa ujumla ambapo inashuhudiwa wananchi wakihamasika kupanda miti

Hapa leo tumeadhimisha siku ya Mama kwa kuendeleza kampeni kabambe ya upandaji miti Tanzania nimefarijika sana kuona wanafunzi wanashiriki kupanda miti hapa na inadhihirisha namna gani nchi yetu imepiga hatua katika mazingira

Aidha, Dkt. Jafo ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na tabia ya ukataji miti hovyo kwaajili ya kuni na mkaa na badala yake watumie nishati mbadala ili kuepuka changamoto za athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Pia, amesema kuwa hivi karibuni Serikali itatoa maelekezo rasmi kwa taasisi mbalimbali kuanza kutumia nishati mbadala kwaajili ya kupikia na kuachana na matumizi ya mkaa na kuni kama ilivyo hivi sasa.

Kwa upande wake Mwakilishi wa mabalozi wa mazingira Bi. Oliver Nyeriga amesema zoezi la upandaji miti lililofanyika katika kituo hicho mbali ya kusaidia kutunza mazingira lakini pia ni njia mojawapo ya kupunguza utegemezi.

Hapa leo tumefanya zoezi la upandaji miti ambalo pia linatufanya tuwe wabunifu zaidi kwani miti hii ya matunda ikikua itawasaidia wanaoishi hapa kujipatia kipato kwa kuuza matunda yatakayopatikana hapa

Bi. Oliver.


Post a Comment

0 Comments