WAFANYABIASHARA wa Jiji la Dodoma wamepata mafunzo na Wizara ya Habari mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhusu matumizi ya anuani za makazi lengo likiwa ni kuelewa utekelezaji wa mfumo huo kuelekea uchumi wa kidijitali.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao kazi hicho Jijini Dodoma Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Aloyce Muogofi amesema kuwa kundi hilo la Wafanyabiashara ni kundi la kimkakati hivyo ni vyema sasa kuwa kidijitali katika ufanyaji kazi zao kama hitaji la Dunia linavyotaka.
Amesema Mafunzo ya Anwani za Makazi yameandaliwa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, yamefanyika kwa jumla ya Wafanyabiashara 100 wa mkoani Dodoma
Amesema matumizi ya anuani za makazi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo nchini ni moja ya njia za kuongeza wateja katika biashara mbalimbali zinazofanywa na wananchi.
Ameeleza wafanyabiashara ni watu muhimu kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na ndio wanaokimbiza uchumi, hivyo wanatakiwa kupewa mafunzo mbalimbali yatakayowasaidia kukuza biashara zao.
Anuani za Makazi ni hitaji la Kidunia, ni ongezeko la orodha ya vitu vinavyotambulisha, kwa Wafanyabiashara ni hatua ya kuongeza wateja bila kutumia nguvu nyingi
Lengo la mfanyabiashara sio tu kuuza biashara alizonazo lakini pia ni namna gani wateja wanaweza kumfikia dunia ya sasa ni ya kibiashara na biashara hizo zinafanyika zaidi kwa kuwasiliana, hivyo kwa kutumia Anwani za Makazi maelekezo yatakuwa ni ya kisayansi, kitaalamu na yatarahisisha utoaji huduma,
Natoa rai kwa wafanyabiashara kuuelewa vizuri mfumo huo kupitia mafunzo mnayopewa ili muweze kuwa mabalozi wazuri na kuweza kuwaelekeza wafanyabiashara wenzao matumizi ya mfumo huo
Naye Mratibu wa Mfumo wa Anwani za Makazi kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Jampyon Mbugi amesema kila kunapokucha, mazingira ya biashara yanabadilika, biashara mtandao sio tu kutoka nchi moja na nyingine au mkoa mmoja na mwingine bali tunatakiwa tufanye biashara mtandao mahali popote.
Ameeleza kwa sasa watu wengi hawana muda wa kufuata bidhaa au huduma mahali, hivyo mfumo huu utasaidia zaidi wafanyabiashara kuwafikishia wateja bidhaa na huduma husika.
Tunatakiwa tunufaike na fursa za uchumi wa kidijitali, hatuwezi kunufaika na aina hiyo ya uchumi bila kuwa na miundombinu au mifumo mbalimbali ikiwemo huu wa Anwani za Makazi
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Habari, Mawasilino na teknolonjia ya habari, Mhandisi Clarence Ichwekeleza amesema kuwa wameamua kutoa elimu hiyo kutokana na wafanyabiashara kuwa wengi na kukutana na watu wengi hivyo kupitia elimu hiyo watakuwa mabalozi wazuri kwa wengine.
Awali akitoa wasilisho kuhusiana na anuani za makazi Muwezeshaji toka Wizara ya Ardhi, Nyumba na maendeleo ya makazi Anold Mkude amesema kuwa kama nchi inahitaji kuwa na anuani za makazi kutokana na Tanzania kuwa mwanachama wa umoja wa mataifa wa anuani za makazi.
0 Comments