WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama amefanya ziara ya kikazi katika taasisi zilizo chini ya ofisi yake ambapo ameanza na Taasisi ya UONGOZI na Watumishi Housing Investments (WHI) kwa lengo la kujiridhisha na utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kama unaendana na fedha iliyotolewa na Serikali kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023 iliyotengwa kuziwezesha taasisi hizo kuwajengea uwezo viongozi na kuwapatia makazi bora watumishi wa umma ili watoe huduma bora kwa wananchi kama ambavyo Serikali ya Serikali ya Awamu ya Sita imekusudia.
Akizungumza na Menejimenti ya taasisi hizo kwa nyakati tofauti, Mhe. Jenista amesema amekutana na Menejimenti ya taasisi hizo ili kufanya tathmini ya utekelezaji wa bajeti kama unaendana na ahadi ya Serikali ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Jenista amesema, ameamua kufanya ziara ya kutathmini utekelezaji wa bajeti kwasababu wakati akiliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya ofisi yake, aliwaahidi Watanzania kuwa, atahakikisha taasisi zote zilizo chini ya ofisi yake zinaitumia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge katika kuboresha Utumishi wa Umma utakaokuwa na tija katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Ili wananchi waendelee kupata huduma bora, Mhe. Jenista ameitaka Menejimenti ya Taasisi ya UONGOZI kuandaa kozi za viongozi za kimkakati ili wajengewe uwezo wa kutekeleza mpango wa maendeleo na mikakati ya kuinua uchumi katika taifa na kuongeza kuwa, Taasisi ya UONGOZI inatakiwa itoe mafunzo yatakayolenga kuinua sekta za utalii na TEHAMA ambazo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amezipa kipaumbele kwa ajili ya maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Bw. Kadari Singo amemhakikishia Mhe. Jenista kuwa mafunzo wanayoyatoa na watakayoendelea kuyatoa yataendelea kuwa yenye ubora unaohitajika katika soko la ushindani.
Katika hatua nyingine, akizungumza na Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) Mhe. Jenista Mhagama ameeleza kuridhishwa na namna taasisi hiyo ilivyotekeleza jukumu la kuanzisha Mfuko wa Faida.
Mmetekeleza vema jukumu la kuanzisha Mfuko wa Faida, na hapa nimeshuhudia takwimu za wananchi waliojiunga na mfuko huo na tayari tumeshaingiza shilingi milioni 300 na wakati huo huo taasisi nyingine za umma ziko kwenye mchakato wa kujiunga na mfuko
Mhe. Jenista
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Watumishi Housing Investments (WHI) Dkt. Fred Msemwa amesema tayari wamepata wawekezaji 2000 waliojiandikisha kwenye Mfuko wa Faida na kati ya hao 500 wameanza kwa kuwekeza shilingi milioni 314.
Dkt. Fred amesema katika kuongeza wigo wa wawekezaji katika mfuko huo, taasisi yake imewasiliana na wawekezaji wakubwa.
Mhe. Jenista baada ya kuhitimisha ziara yake katika taasisi hizo mbili, atatembelea Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuendelea na tathmini ya utekelezaji wa bajeti katika Mfuko huo.
0 Comments