WAKALA wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu ADEM imesema kuwa imejipanga kutoa Mafunzo ya Uongozi na Usimamizi wa Shule kwa Walimu Wakuu wapatao elfu 17,000 mafunzo hayo yakiwa na lengo la kutoa mafunzo ya utawala bora kwa wasimamizi wa elimu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu ADEM Dkt Siston Mgullah wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa majukumu ya wakala huo na vipaumbele vyake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema Katika kipindi cha mwaka 2021/2022, Wakala umeweza kushirikiana na mashirika mengine katika kutoa mafunzo ya Uongozi, Usimamizi na Uthibiti Ubora wa Elimu ikiwemo UNICEF, EQUIP-TZ, World Bank, GPE-LANES, PS3+, Good Neighbors (TZ, Zanzibar Office), Mwanamke Initiatives Foundation (MIF), Aga Khan University (AKU, IED, EA) na Shule Bora.
Aidha amesema malengo mengine ya wakala kwa mwaka 2022/2023 ni pamoja na Kudahili Walimu 2343 katika Kozi za CELMA, DEMA na DSQA, kuandaa Kiongozi cha Mwalimu Mkuu na kuandaa Mwongozo wa Utawala Bora kwa viongozi wa Serikali za Mitaa.
Malengo yetu ni kuimarisha usimamizi wa utoaji wa elimu bora shuleni kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ya elimu, kuziba ombwe la maarifa na ujuzi ambalo kiongozi au mtendaji hakupata katika mafunzo ya awali ya Ualimu na kuongeza idadi ya viongozi wenye maarifa ya uongozi na usimamizi wa elimu
Katika kipindi cha mwaka 2020/2021, Wakala umefanya tafiti mbalimbali zikiwemo za tathimini ya matokeo ya Mafunzo ya KKK kwa Walimu wa Darasa la III na IV yaliyofanyika Tanzania Bara, utekelezaji wa uthibiti ubora wa shule na utoaji wa mrejesho kwa walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji katika shule za Msingi
Dkt Mgullah
Akizungmzia Kuhusu mafunzo kwa njia ya masafa, amesema kwa sasa wana mradi na Chuo kikuu cha Mzumbe kilichopo Morogoro kwa ajili ya kuandaa Moduli za kuendeshea mafunzo ya masafa.
Akizungumzia kuhusu Ufuatiliaji wa utendaji kazi wa Wakuu wa Shule waliopata mafunzo ya Uongozi na Utawala katika Elimu, ufuatiliaji wa matokeo ya mafunzo ya Stashahada ya uongozi na usimamizi wa Elimu na tathmini ya athari za kozi ya Astashahda ya Uongozi, Usimamizi na Utawala wa elimu iliyofanyika katika mikoa minne.
Katika kipindi cha miaka mitano (2018- 2022), Wakala umetoa machapisho ya Moduli ya wajibu na majukumu ya Mjumbe wa Kamati na Bodi ya Shule, Wajibu na majukumu ya Mjumbe wa Bodi ya Chuo cha Ualimu 2022 Moduli ya uthibiti ubora wa Shule wa ndani 2021 na uandaaji na usimamizi wa Utekelezaji wa Mpango wa Jumla wa Maendeleo ya Shule - 2018
UTEKELEZAJI WA MALENGO
Amesema Wakala umedahili Walimu 1,839 katika mafunzo ya Stashahada ya Uongozi na Usimamizi wa Elimu (DEMA) na Stashahada ya Uthibiti Ubora wa Shule (DSQA) ili kuwapa ujuzi na maarifa walimu katika usimamizi, ufuatiliaji na tathimini katika elimu.
Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani, kwa Maafisa 3,860 (REOs, RAOs, DEOs, WEOs) ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji wenye kuleta tija katika elimu,
Wakala umetoa mafunzo ya muda mfupi kuhusu uthibiti ubora wa shule wa ndani kwa walimu 7,612 ili kuwajengea uwezo wa kusimamia ufundishaji na ujifunzaji katika shule wanazosimamia Wakala umeendesha mafunzo ya muda mfupi kwa Walimu Wakuu na Waratibu wa Taaluma 147 kutoka katika Shule za Msingi na Sekondari Zanzibar, chini ya mradi wa Mwanamke Initiative Foundation (MIF).
Dkt Magullah amesema Wakala umeendesha mafunzo ya Kamati za Shule kwa Washiriki 126 katika Mkoa wa Songwe ili kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika Shule na umeandaa mtaala wa shahada ya menejimenti ya uthibiti ubora wa elimu ili kuimarisha usimamizi na utoaji wa elimu bora katika ngazi zote za elimu.
Amesema Wakala umefanya Tafiti sita na kuwasilishwa kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kubaini mapungufu na kuandaa mafunzo wezeshi kwa wahusika, wakala umeandaa Moduli 3 katika eneo la Uongozi na Usimamizi wa Shule ili kuendesha mafunzo ya kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji wa ujenzi wa umahiri kwa walimu wa Shule za Sekondari Zanzibar na umeandika vitabu vya kujenga umahiri katika utekelezaji wa Mtaala wa Sekondari ili kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza kwa ajili ya Shule za Zanzibar.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu Wa Serikali Gerson Msigwa amesema Serikali inaweka fedha nyingi kwenye sekta ya elimu nchi nzima ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/23, sekta ya elimu pekee imetengewa Shilingi trilioni 5.8. Chuo hiki ni moja ya juhudi za Serikali za kusimamia ubora wa elimu.Fedha hizi ni nyingi ambazo zinahitaji usimamizi wa karibu, hivyo wale viongozi wa kwenye taasisi zinazosimamia elimu lazima wawe na ujuzi na mbinu nzuri za kusimamia maendeleo ya elimu ili tuweze kupata thamani ya fedha zilizotolewa na Serikali
Viongozi wanaosimamia Taasisi za Elimu wanatakiwa wakasome katika chuo hiki ili wakapate ujuzi wakasimamie vizuri taasisi hizo. Natoa wito kwa waajiri kutosita kuwaruhusu viongozi wa taasisi za elimu kwenda kusoma ADEM
Msigwa.
0 Comments