📌RHODA SIMBA
Maeneo mbalimbali duniani yamekuwa yakikabiliana na changamoto ya ukatili wa kijinsia. Hata hivyo, changamoto hiyo, licha ya jitihada zinazofanywa, lakini bado inaonekana kushika kasi.
Mathalan, nchini Tanzania, ripoti bado zinaonesha kwamba asilimia 40 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamewahi kufanyiwa ukatili wa kimwili au kingono mara moja au zaidi katika maishani yao. Hii ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum mwaka 2021.
Miongoni mwa wanawake walliokabiliwa na masaibu hayo nchini Tanzania ni pamoja na Zilipa Zebadayo, 39, mkazi wa kijiji cha Nagulo kilichopo Wilayani Chamwino Mkoani Dodoma.
Akimwelezea mwandishi wa makala hii, Zilipa anasema yeye amewahi kuolewa akiwa na umri wa miaka 19 na mwanamume aliyemzidi umri.
Anasema chanzo cha kuolewa kwake ni kutokana na hali ngumu ya maisha na kukosa kitu cha kujishughulisha. Na hili limetokea pindi tu alipomaliza darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo. Kama ilivyo kwa idadi kubwa ya wasichana wanaomaliza kusoma na kushindwa kuendelea, nae alienda jijini Dar es Salaam kama mfanyakazi wa ndani.
Nilichoka kufanya kazi za ndani nikaonanirudi nyumbani ili nipate mchumba niolewe. Nikapata mchumba wa hapa hapa kijijini kwetu, tukafunga ndoa mwaka 1999. Baada ya wiki tu, vipigo vikaanza. Nilikuwa napigwa mpaka nazimia. Halafu majirani zangu wote walikuwa wanaogopa kuja kuamua ugomvi wetu nikianza kupigwa
Zilipa
Taarifa hiyo imeongeza kusema kuwa asilimia 20 ya wanawake wamefanyiwa ukatili wa kimwili huku asilimia 9 ya umri kati ya miaka 15 hadi 49 wameingiliwa kimwili bila ridhaa yao.
Wakati huo huo, imearifiwa kwamba, katika jamii baadhi ya malalamiko hayo ya ukatili wa kijinsia hayaripotiwi na baadhi mengine kutosikilizwa au kufanyiwa kazi pindi yanapotolewa.
Zilipa anasema hali hiyo ya manyanyaso na kipigo iliendelea mpaka akaja akapata ujauzito wa mtoto wake wa kwanza anasema aliwahi kupigwa mpaka mimba ikataka kuharibika.
Mimba iitaka kuharibika ya mwanangu wa kwanza yani kuna wakati unapigwa tuu unakuta ana visababu vingi mfano mbona mboga ina mafuta ugali haujaiva, kwa kweli nimepitia kipindi kigumu mno nikaja nikajifungua mtoto wa kwanza sijapumzika nikapata ujauzito wa pili hali ikaendelea akaja akanipiga mpaka akaning’oa meno yangu mawili ya mbele nikaenda kuripoti ofisi ya serikali za mtaa wakasuluhisha ile kesi tukafika mahakani tukaja kukubaliana tuachane ila atimize wajibu wake wa kutoa huduma kwa watoto, basi mpaka sasa ameendelea na maisha yake nami pia sema ndio hivyo kaniachia kilema cha kutokuwa na meno ya mbele
Zilipa.
Lakini sio wote wenye ujasiri wa kutoa taarifa kama aliokuwa nao Zilipe. Elice Chigataa, 50, ambaye ni mama wa watoto watano nae yalimpata kama ya Zilipa.Mama huyu ambae ni mkazi wa kijiji cha Nghambi kilichopo Wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, anasema yeye aliwahi kuolewa na kuishi na mumewe kwa muda wote mpaka anafariki, lakini alikuwa akipitia ukatili wa kupigwa hadi kuchomwa na moto na hakuwa na uelewa wapi anaweza akaenda kusema.
Nilikuwa napigwa. Anachukua moto wa kuni ananichoma mikononi, lakini kila nikikimbia kwetu. akija anasema atabadilika, narudi kuishi nae, lakini habadiliki. Mkikaa siku mbili akilewa tu anaanza tena ukorofi na ananambia utaenda wapi ukisema polisi nitakupiga nikuuwe kwa hiyo nikawa sielewi wapi pakusemea matatizo yangu. Nimeteseka kwa kipindi hiki chote mpaka kifo kilipokuja kumchukua,
Elice.
Baadhi ya wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, wanakiri kwamba, uhaba wa elimu miongoni mwa waathirika kutojua wapi watoe taarifa ni moja wapo ya changamoto, lakini pia kukosa ujasiri.
Hata hivyo, suala la ukatili halipo kwa wanawake pekee, ripoti mbalimbali zinaonyesha wanaume pia ni waathirika. Ingawa wanaume wanaona aibu kuripoti wanapofanyiwa vitendo vya ukatili. Hii pia inatokana na fikra hasi za watu kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kwa sababu jamii nyingi hazizungumzi kuhusu ukatili kutokana na uwepo wa mila na desturi na mifumo dume.
Ndewa Elia ni mwanamke mwenye umri wa miaka 37 mwenye watoto watano mkazi wa kijiji cha Nkulabi kilichopo jijini Dodoma anasema chanzo cha yeye kufanyiwa ukatili na mume wake, ni baada ya mumewe kukaidi ushauri wa wataalamu wa afya wa kumtaka yeye ajifungue katika hospitali ya rufaa.
Alikataa niende kujifungua mjini kwa madai kwamba gharama za mjini ni kubwa. Baada ya kumlazimisha akanambia sikuzikikaribia nitaendea, basi nikasubiri siku zimeenda kila nikimkumbusha anakuwa mkali, mpaka siku nimeumwa uchungu usiku akaniacha akanifungia ndani akaondoka.
Usiku ule nilipata uchungu wa uzazi mpaka nikajifungulia ndanii peke yangu. Nilipiga kelele majirani zangu wakaja kunisaidia usiku ule huku wakiniuliza mumeo yukwapi nikawaelezea hali halisi
Ndewa
Baada ya kupata msaada huo, Ndewa alishauriwa na majirani kwenda kutoa taarifa polisi, lakini kwa masikitiko, anasema, alihuzunishwa na majibu aliyoyapata polisi.
Niliambiwa nitoe hela ili kesi iweze kuendelea. Niliposema sina hela kwa sababu nimetoka kujifungua, nikaambiwa nikapumzike
Baada ya kuwa mwanangu amekuwa kidogo nikarudi tena kituoni kuulizia wakaniambia wao hawasuuhishi wala kuachanisha mke na mume turudi tukazungmze na kuyamaliza nyumbani
Ndewa.
Kauli ya polisi kuhusiana na tuhuma za rushwa pale jamii inapoenda kuripoti tukio la ukatili inasema huduma hiyo inatolewa bure bila malipo na endapo mwananchi akafika kituo cha polisi na akakutana na askari anaekiuka maadili akataka rushwa apige simu bure ya polisi ya 113.
Wanaharakati wa kupinga ukatili wa jinsia wanazungumza
Zakia Msangi ni mwanasheria kutoka Shirika la Wanawake linalotumia sheria kumuokoa mwanamke na mtoto anayepitia ukatili wa kijinsia WILDAF.
Shirika lao muda mwingi limekuwa
likipambana na masuala ya kupinga kwa kiasi kikubwa ukatili wa kijinsia
na ndoa za utotoni kwa kutoa elimu kwa jamii kwa njia ya matamasha.
Zakia anasema mfumo wa kuripoti taarifa za ukatili wa kijinsia ni rafiki kwa jamii kwakuwa sasa kuna madawati ya jinsia kwenye vituo vya polisi wanaosikiliza na kuhudumia kesi hizo.
Mfumo ni rafiki sema tunachoendelea kusisitiza jamii ione suala hili la kuripoti ni suala la kawaida si kitendo cha aibu na kwa sasa kuna Ofisi za Ustawi wa Jamii zilizoko kila kata hasa kwenye kesi hizi za ukatili wafike kutoa taarifa zao
Zakia.
Akizungumzia kuhusu mchango wa WILDAF anasema wao wanatoa msaada wa kisheria kwa wahanga ambao tayari wamefanyiwa vitendo hivi vya ukatili wa kijinsia bure bila malipo yoyote.
Naomi Gerald ni Afisa Miradi Kutoka Shirika la Rafiki lililopo
Mkoani Shinyanga anasema ili kukabiliana na vitendo hivyo vya ukatili wa
kijinsia wao wanatoa elimu za jinsia kwa vikundi ambavyo
wamewawezesha mabinti kwa ajili ya kujikwamua Kiuchumi.
Tunawatengenezea vikundi hivi ili kuepukana na vitu ambavyo vitawapeleka kwenye ukatili wa jinsia unajua kitendo cha kukosa kitu cha kujishughulisha nacho Moja kwa Moja hata akienda kuolewa atanyanyasika.
Sisi kama Rafiki tumewatengenezea mabinti biashara ya kukopeshana wanatengeneza sabuni,karanga mikoba Ili wajipatie vipato na kupitia miradi ambayo tunaifanya hizo kesi zipo na tulitambua kuwa hilo tatizo lipo na ndio maana tunaenda kupambana nalo kwa kuwapa mtaji mabinti wafanye ujasiriamali
Jamii iendelee kutoa ushirikiano kwa mashirika haya ambayo yanafanya harakati za kupinga ukatili iwe tayari kufikiwa na kupata elimu kwaajili ya kujikinga na kupata elimu juu ya ukatili
Kwa kiwango kikubwa sisi tunakutana na wazazi kupitia vijiwe mbalimbali ikiwemo vijiwe vya kahawa tunawapatia Elimu kuhusu kupinga ukatili pamoja ndoa za utotoni pia tunawaelimisha mabinti.
Nini kauli ya dawati la jinsia?
Christer Kayombo ni Mkuu wa Dawati la Jinsia na watoto Mkoa wa Dodoma anasema kasi ya kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia kwa sasa imekuwa kubwa tofauti na hapo zamani ambapo watu walikuwa wakinyamaza pale wanapofanyiwa ukatili.
Sisi kama dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma vitendo hivi vya ukatili vinaripotiwa na ili kukabiliana na tatizo hili la ukatili kwanza kabisa tunaendelea kutoa elimu ya aina ya makosa ambayo mtu ama jamii ikifanyiwa ione kabisa kuwa ni ukatili wa kijinsia
Tunatoa elimu kwenye jamii, shule za sekondari, msingi, vyuo mbalimbali. Tunatoa elimu kwenye vyuo kwa sababu huko bado kuna watoto na ili kukomesha vitendo hivi sisi kama dawati la jinsia mkoa tunapeleleza kesi hizi kuanzia tukio lilipotendeka hadi hatua za mahakamani. Tunafanya kazi kwa weledi na ufanisi kuharakisha upepelezi. Tunafungua hizi kesi katika madawati yetu kwa usiri Ili tuweze kupata taarifa muhimu ili ziweze kutusaidia
Kayombo.
Kayombo anasema jamii inaishi na waharifu ambao tayari walishawafanyia watu ukatili lakini hawajafikishwa popote, na anaongezea kuwa wao kama dawati la jinsia wanataka kazi wanayoifanya jamii ione kuwa mtuhumiwa kafungwa miaka 30 au kifungo cha maisha.
Wito wangu kwa jamii itoe ushirikiano, wanapoona viashiria hivi vya ukatili wa kijinsia waripoti kwani jeshi la polisi haliwezi kutabiri na waache ile tabia ya kumaliza kesi zao majumbani. Hii inawaumiza waathirika waliofanyiwa vitendo vya ukatili
Kayombo
0 Comments