KUFUNGUKA KWA FURSA ZA KIUCHUMI KUMEWEZESHA WADAU WA MAENDELEO YA JAMII KUPATA AJIRA.

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

WAKATI suala la ajira likiwa changamoto kwa baadhi ya wahitimu imeelezwa kuwa kufunguka kwa fursa za kiuchumi kumewezesha wahitimu wa taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru kupata ajira katika makampuni ya biashara na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dodoma wakati akiwasilisha utekelezaji na mwelekeo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mkuu wa Taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru Dkt. Bakari George amesema upanuzi wa fursa mbalimbali za mikopo ya serikali na kutoka sekta binafsi kumewezesha baadhi ya wahitimu kujiajiri na kuajiri wengine. 

Tunamshukuru Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kufungua milango ya ajira ambazo zimewezesha baadhi ya wahitimu wetu kuajiriwa kama Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wahadhiri, Watendaji wa Kata na Vijiji, Maafisa Mikopo na wengine wameajiriwa kwenye vyombo mbalimbali ya Ulinzi na Usalama

 Dkt Bakari amesema kwa mwaka wa Fedha 2022/2023, Taasisi inatarajia kuongeza program 6 za mafunzo zinazotarajiwa kuanza kutolewa dirisha la Machi 2023 ambapo maandalizi ya program hizi yamezingatia mahitaji ya soko la ajira kwa sasa na umuhimu wa kuandaa wahitimu wenye fikra sahihi na uwezo wa kujiajiri. 

Ameongeza kuwa Taasisi hiyo inaendesha program 15 za mafunzo, kwa kipekee, mitaala inayotolewa na Taasisi imezingatia uwiano kati ya nadharia na vitendo. Hivyo mitaala yote inatekelezwa kwa kuzingatia dhana tatu ambazo ni uanagenzi, ushirikishwaji jamii na uanagenzi.

Ongezeko la udahili linachagizwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika uimarishaji wa elimu kwa ngazi za msingi na sekondari na umuhimu wa fani ya maendeleo ya jamii katika muktadha wa upatikanaji wa ajira na mawanda mapana ya kuwezesha wanafunzi kukabiliana na changamoto za soko la ajira

Kuhusu juhudi za serikali za kuimarisha mazingira ya ujifunzaji kwa wanafunzi wa kike hapa nchini, amesema Taasisi ya maendeleo ya jamii Tengeru iliyopo Jijini Arusha kwa mwaka wa fedha 2022/2023 imeipata shilingi Bilion 2.3 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la kike ambalo litasaidia kuondoa changamoto wanazokabiliana nazo ikiwemo vitendo vya ubakaji .

Pia amesema kuwa taasisi hiyo imeanzisha utaratibu wa kuwachangia fedha wanafunzi wanaoishi mazingira magumu huku akiwataka watanzania watakaowiwa kutoa michango yao ili wanafunzi hao waweze kutimiza malengo yao .

Kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2020/2021, Serikali ya Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan illipatia Taasisi jumla ya Shillingi 2,700,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa kumbi pacha za mihadhara yenye uwezo wa kuchukua idadi ya wanafunzi 1008 ikiwa ni wanafunzi 504 kwa upande mmoja na hosteli ya wasichana ya ghorofa nne yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kike 568.

Kwa upande wake Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa elimu tayari imeajiri maafsa maendeleo ya jamii 3000 huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya elfu tano ili jamii iweze kufikiwa na wataalamu hao.

Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru inatoa mafunzo ya elimu ya juu na kati na inatekeleza majukumu ya kuendesha mafunzo ya muda mrefu na mfupi katika nyanja ya Maendeleo ya Jamii, Upangaji na Usimamizi wa Miradi na Jinsia na Maendeleo pamoja na kufanya tafiti na kutoa ushauri elekezi katika masuala ya maendeleo ya jamii na ustawi wa watu kwa ujumla

  

 

Post a Comment

0 Comments