Tina Aloyce (si jina lake halisi), kutoka kijiji cha Ngwenda Wilaya
ya Chamwino, Mkoa wa Dodoma ni msichana aliyeozeshwa akiwa na umri wa
miaka 15 tu, anasema hakuwa na maamuzi, wazazi wake waliamua kumuozesha
akiwa na umri huo ili fedha ya mahari itakayopatikana iweze kuhudumia
familia nyumbani.
“Mimi niliishia darasa la tano tu, maisha nyumbani yalikuwa magumu
sana, kuna muda nilikuwa nakosa mahitaji ya shule kama vile sare, vitabu nk.
Hapo ndipo nilipoona hakuna haja ya mimi kuendelea na masomo nikaacha
shule,” anaongea Tina huku akiwa ameshika tama machozi yakiwa yana
mlengalenga.
Kwa mujibu wa mtandao wa kutokomeza ndoa za
utotoni nchini TECMN umebainisha kuwa umasikini au
hali duni ya kaya nyingi nchini, imekua inachangia ongezeko la ndoa
za utotoni kwa wasichana chini ya miaka 18.
TECMN
inasema Mkoa wa Dodoma una kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni.
Takwimu zinaonesha Dodoma ina asilimia 51 ya ndoa za utotoni kwa
Tanzania.
Tina anasema chanzo cha yeye kuacha shule mpaka kufikia
kuolewa katika umri huo mdogo ni hali duni ya familia yao.
“Nikaacha shule nikawa namsaidia mama shughuli zake za
nyumbani za kilimo na biashara yake, mama alikuwa anauza pombe za
kienyeji, akajitokeza mwanaume akasema anataka kunioa, baba na mama wakaridhia wakampangia
mahari, akatoa akanioa,” anaelezea Tina kwa masikitiko.
HALI YA NDOA
Akizungumzia hali ya maisha yake baada ya ndoa anasema
hakuwahi kufurahia ndoa hiyo alikuwa akipitia maisha magumu ya unyanyasaji
huku akisema hali ile anadhani ilikuwa inatokea kwasababu ya umri
wake mdogo na kutokuwa na uelewa juu ya maisha.
“Nilikuwa napigwa, anakata fimbo nikifanya kosa hata liwe
dogo tu ananichapa. Nikapata ujauzito, kujifungua kwangu kulikuwa kwa shida
sana. Kutokana na umri wangu mdogo, baada ya kujifungua manyanyaso
yaliendelea ikabidi nitoroke na kurudi nyumbani kwa wazazi wangu.
“Mpaka sasa najutia, natamani ningesoma na mimi nipange maisha
yangu kama watu wengine. Baada ya kurudi hapa nyumbani, nashukuru wazazi
walinipokea. Siku hizi nafanya kazi ya mama lishe ambayo inanisaidia kuingiza
kipato na kumhudumia mtoto wangu. Wito wangu kwa wasichana wenzangu, wasome na
wazazi nao waache kutuozesha katika umri mdogo. Si unaona maisha nayoyapitia
mimi?” anasema Tina, machozi yakimlengalenga.
Ripoti
ya tathmini ya mwaka 2018 iliyotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la
kuhudumia watoto- UNICEF inaonyesha kwamba huenda kukawa na ndoa nyingine za
utotoni milioni 10 kabla ya kumalizika kwa muongo huu.
Shirika hilo limeeleza kuwa takribani ndoa za utotoni milioni 25
zimezuiwa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita ambapo kwa sasa, mtoto mmoja
kati ya watano wanaolewa kabla ya umri wa miaka 18 ukilinganisha na mmoja kati
ya wanne aliyekuwa anaolewa kipindi hicho.
Aksa Masigazwa (Si jina halisi) ni msichana mwenye umri wa
miaka 17 kutoka kijiji cha Nhinhi kilichopo Wilaya hiyo hiyo ya Chamwino,
naye anasema chanzo cha kuolewa kwake ni tamaa ya wazazi kutaka kumiliki
mifugo mingi kwa haraka.
“Mimi nilisoma mpaka darasa la saba nilivyomaliza tu, wazazi wangu
wakaniambia niolewe na mtoto wa jirani yetu ambae alikuwa akimiliki mifugo
mingi. Baba akachukua mahari ya ng’ombe, mbuzi na kondoo.
Nikaolewa. Kwa kweli sikufurahia kuolewa. Natamani na mimi
ningeendelea na masomo kama wengine. Ndoto yangu ndio iliishia pale, hapa
nilipo mimi kwa sasa ni mkulima, nilitamani nami nisome nimalize niweze kupanga
maisha yangu,”anasema Aksa.
UNICEF inasema kuwa mmoja kati ya
watoto watatu wanapitia ndoa za utotoni kwa kipindi hiki Afrika ukilinganisha
na mmoja kati ya watoto watano waliokuwa wakiolewa miaka kumi iliyopita.
WAZAZI WAFUNGUKA
Elias Matonya (si jina lake halisi) mkazi wa kijiji cha Nghwenda
kilichopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma ni mzazi aliyewahi kumuozesha mtoto
wake akiwa katika umri mdogo, anasema yeye hakuwa na uelewa ya kuwa mtoto wa
kike pia anapaswa kusoma kama alivyo mtoto wa kiume.
“Maisha yetu hapa kijijini nilichokuwa naamini mtoto wa kike
akiolewa anaweza wasaidia wenzake. Mimi nilimuozesha mtoto wangu akiwa na umri
wa miaka 15. Hapa nyumbani nina watoto tisa, ile mahari ilinisaidia kuwahudumia
wadogo zake mahitaji ya hapa nyumbani.
“Kumbe sikuwa nafahamu kwamba mtoto wa kike akisoma anaweza
kuikomboa familia zaidi ya nilivyokuwa nafikiria, matokeo yake mtoto kawa
ananyanyasika akarudi hapa nyumbani nikawa nawahudumia wote yani nikapata kazi
mara mbili ya kulea watoto wawili,”anasema Matonya.
Julius Mhembano ambae naye hakutaka jina lake litajwe kutokana na
sababu za kiusalama, ni mzazi pia aliyewahi kumuozesha binti yake akiwa katika
umri mdogo, anasema yeye hakuwa na changamoto ila aliamini akimuozesha
mtoto wake ataongeza mifugo.
“Mimi fahari yangu ilikuwa kuona zizi langu limejaa ng’ombe, mbuzi
na kondoo. Niliwahi kuwaozesha watoto wangu wa kike watatu, mmoja alikuwa na
miaka 14, wa pili miaka 13 na mwingine alikuwa na miaka 16, na kweli nilijaza
zizi langu mifugo bila kujua kuwa nawakosesha watoto wangu haki za kusoma na
kupanga maisha.
“Huwa najuta kuona watoto wa wenzangu wamesoma wana maisha
mazuri mimi wangu wapo wanaishia kuteseka. Natoa wito kwa wazazi
wenzangu wasidanganyike. Wawapeleke watoto shule kwa sababu watoto wa kike
pia wana haki,” anasema Mhembano.
Zakia Msangi ni mwanasheria kutoka shirika la wanawake
linalotumia sheria kumuokoa mwanamke na mtoto anayepitia ukatili
wa kijinsia WILDAF. Anasema shirika lao muda mwingi limekuwa likipambana
na masuala ya kupinga kwa kiasi kikubwa ndoa za utotoni kwa kutoa elimu
kwa jamii kwa njia yamatamasha pamoja na vyombo vya habari, kwa kuzingatia
sheria.
“Sheria ya mtoto ipo na imeeleza kabisa mtoto ni yule alie chini
ya miaka 18 na haki za mtoto wajibu, lakini tunayo sheria ya ndoa ambayo
inakinzana na kifungu hiki cha miaka 18 cha mtoto ambapo kifungu cha 13 na
17 cha sheria ya ndoa ya mwaka 1971 imeridhia mtoto wa kike aweze
kuolewa akiwa na umri wa miaka 15 na 14 kwa ridhaa ya mahakama. Sasa
tunashangaa, sheria imemkubali mtoto ni chini ya miaka 18 sasa hii ya sheria
bado inaruhusu mtoto wa miaka 15 aolewe sisi tunaendelea kuipigia kelele
sheria hii kwa kutoa maoni.
“Tumeandika vifungu vyenye shida ikiwemo na hiyo ya ndoa na tumepeleka
haya mapendekezo bungeni pamoja na Wizarani kuweza kupaka mabadiliko
haraka iwezekanavyo” anasema Zakia
Anasema WILDAF imejikita katika sheria zaidi kwa
sababu tayari ndoa za utotoni zipo na zinaendelea mtaani
“Tunaendelea kukemea kwa sababu madhara ni makubwa wanayoyapata
watoto katika ndoa hizi za utotoni. Wengi hawapo tayari kiakili, kimwili na
kimfumo kuweza kupokea majukumu mazito ya ndani ya ndoa. Watu wazima bado ndoa
zinawashinda sembuse huyu mdogo ambaye anatakiwa acheze na watoto
wenzie tayari tunamvika majukumu makubwa ya kulea familia wakati umri wake
bado, tunakosea,” amesema Zakia.
Naomi Gerald ni Afisa Miradi kutoka Taasisi isiyo ya
kiserikali ya Rafiki Social Development Organization (RAFIKI SDO) iliyopo mkoani
Shinyanga, Nayo imejikita katika masuala ya kupinga ndoa za
utotoni, mimba za utotoni, afya pamoja na elimu.
Naomi anasema mbinu moja wapo ya kupambana na hali hiyo ni
kukutana na wazazi pamoja na mabinti wenyewe ili kuwapatia elimu.
“Kwa
kiwango kikubwa sisi tunakutana na wazazi kupitia vijiwe mbalimbali ikiwemo
vijiwe vya kahawa tunawapatia elimu kuhusu kupinga ndoa hizi za utotoni pia
tunawaelimisha mabinti wenyewe, tunawapatia elimu pia ya masuala
ya uzazi wa mpango akipata ile elimu basi hapati tena ile changamoto
ambayo iliwahi mpata kwa wale ambao tayari wamepitia,” anasema.
“Tumefanikiwa
kuwawezesha mabinti kwa kuwatengenezea vikundi vya kujikwamua kiuchumi ambavyo
vinawakopesha nao wanafanya biashara ndogondogo ikiwemo kutengeneza
sabuni, kupika karanga ili wajipatie kipato na hiyo inawaepusha na
vishawishi ambavyo vinaweza kuwaingiza katika ndoa za utotoni,” anasema
Naomi.
Anasema hizo
kesi zipo na wanaendelea kutoa elimu kwa jamii huku akitoa rai kwa
wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mashirika ambayo yanafanya harakati za
kupinga ndoa hizi za utotoni.
“Jamii
iwe tayari kufikiwa na kupata elimu kwa ajili ya kujikinga na masuala haya
ya ndoa za utotoni kwa sababu asilimia kubwa hali duni ya
maisha katika familia inawafanya watoto wa kike waolewe mapema, akipata
mwanaume ambae atakuwa anampatia pesa kidogo basi ni rahisi kuingia kwenye ndoa
hizo ili mradi tu amhudumie hali duni aliyonayo,” anasema Naomi.
Kuhusu muswaada wa kutaka kuongeza umri
wa kuolewa kwa mtoto miaka 21 Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria
inasema inaendelea na zoezi la kukusanya na kuchambua maoni
yakikamilika Wizara itawasilisha Bungeni mapendekezo ya
marekebisho ya sheria hiyo ya ndoa.
Aidha kabla ya maamuzi hayo
serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kutunga sheria
mpya na kurekebisha sheria mbalimbali zinazohusiana na upingaji wa
ukatili wa kijinsia na umri wa mtoto.
Sheria hizo ni pamoja na kutoa tafsiri
ya mtoto katika sheria ya mikataba sura ya 345 kwa kuelezea umri
sheria sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 ambayo ilitoa tafsiri
mtoto ni mwenye umri wa miaka 12 hadi 18 na hivyo akizidi umri huo anakuwa ni
mtu mzima, sheria ya ndoa hususani vifungu vya 13-17 vya sheria ya ndoa ya
mwaka 1971 ambavyo vimeweka bayana kuwa mtoto wa kike anaweza kuolewa
akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi au umri wa mahakama.
Michael
Chigataa ni Afisa Mtendaji wa kata ya Ngwenda iliyopo Wilayani Chamwino
mkoani hapa, anasema ndoa za utotoni katika kata yake zipo lakini si
nyingi kutokana na jamii kutokuwa na elimu/uelewa wa kutoa taarifa katika
ofisi za serikali za mtaa wakihisi kuwa si sahihi .
“Kesi za mimba na ndoa za utotoni zipo hapa kwenye kata yetu, ila jamii bado
haitoi taarifa ya watuhumiwa lakini sisi tunachofanya tukisikia tetesi tunaenda
kufuatilia mpaka tunampata mtuhumiwa na kumfikisha sehemu husika na sisi
tunaendelea kutoa wito kwa jamii isivifumbie macho vitendo hivi pale
vinapotokea watoe taarifa ili wahusika wachukuliwe hatua,”anasema
Chigataa.
Naye
Samweli Lungwa Mwenyekiti wa mtaa wa Mazengo uliopo katika kijiji cha Nkulabi Wilaya
ya Dodoma mjini anasema elimu inaendelea kutolewa kwa jamii kuhusu madhara
ya mimba na ndoa za utotoni sambamba na kuwataka wananchi watoe
ushirikiano pale yanapotokea matukio haya.
“Jamii
tunayoishi imezoea masuala ya kumalizana wao kwa wao mfano familia ya mzee
fulani kijana amempa mimba mtoto, wazazi wanaenda kukaa na kuyamaliza wenyewe
bila kushirikisha viongozi wa mtaa hii hali inatuharibia watoto na inazima
ndoto za watoto walio wengi”anasema Lungwa.
DAWATI LA JINSIA.
Christa
Kayombo ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi na Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto
Polisi Dodoma anasema Dawati linaendelea kukabiliana na kutokomeza
ndoa za utotoni kwa kutoa elimu katika shule ya msingi, sekondari, vyuo pamoja
na watoto waliopo chini ya miaka 18.
“Tunatoa elimu kwa mtu yoyote ambae yupo
chini ya miaka 18 tunaelimisha jamii kwamba mtu mwenye umri wa miaka 18
ukifanya naye mapenzi unakuwa umembaka na kama mtu yoyote atapewa mimba akiwa
chini ya miaka 18 tunafungua kosa la kubaka, kwa sababu ndoa hiyo itakuwa
imetokea kutokana na kitendo cha kubakwa, japo kuna wengine wanadhani
wakikubaliana anakuwa hajabakwa lakini sisi tunasema akikubali ni amekubali kwa
sababu ya utoto wake mtu mzima umemrubuni kwa kutumia udhaifu wake wa
utoto”amesema Kayombo
Kayombo anasema ndoa za utotoni na vitendo
vya ubakaji vinaripotiwa kwenye madawati na ni dhahiri kwamba tatizo
hilo lipo katika jamii na idadi ya wanafunzi wanaopata mimba za
utotoni wapo anasema Jeshi la Polisi mchango wake umekuwa ni mkubwa katika
kufatilia kesi mara tu tatizo hilo linapogundulika.
“Ili kukomesha vitendo hivi sisi kama dawati
la Jinsia Mkoa tunapeleleza kesi hizi kuanzia tukio lilipotendeka hadi hatua za
mahakamani, tunafanya kazi kwa weledi na ufanisi na kuharakisha upepelezi
tunafungua hizi kesi katika madawati yetu kwa usiri ili tuweze kupata taarifa
muhimu ili ziweze kutusaidia” anasema Kayombo
Aidha Kayombo anatoa wito kwa jamii
iendelee kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pale yanapotokea matukio
ya ndoa hizo kwa kutoa taarifa na kusema kuwa jamii iache mazoea ya kumaliza
kesi wenyewe.
“Sisi tunafanya kazi tunataka jamii ione kuwa mtuhumiwa aliyefanya kosa anafungwa miaka 30 au kifungo cha maisha mara baada ya kukutwa na hatia, tunaomba jamii itupe ushirikiano, Jeshi la polisi haliwezi kutabili na jamii tunaiomba iache tabia ya kumalizana wenyewe kwa wenyewe kwani kwa kufanya hivyo tunafuga waharifu na wataendelea kuwa kwenye jamii”anasema Kayombo
0 Comments