TAKUKURU YATAKIWA KUFANYA UCHUNGUZI WA MATUMIZI YA FEDHA ZA TASAF ZILIZOTOLEWA KUJENGA ZAHANATI KATIKA KIJIJI CHA MTAKUJA

 ðŸ“ŒJAMES K. MWANAMYOTO

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka Kamanda wa TAKUKURU Wilayani Ruangwa kufanya uchunguzi wa matumizi ya kiasi cha shilingi 102,080,357.14/= zilizotolewa na Serikali kupitia TASAF ili kujenga Zahanati katika Kijiji cha Mtakuja Wilayani Ruangwa na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi huo kwake kabla ya kuhitimisha ziara yake mkoani Lindi.

Mhe. Ndejembi ametoa maelekezo hayo kwa kamanda wa TAKUKURU Wilaya ya Ruangwa mara baada ya kukagua na kutoridhishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Kijiji cha Mtakuja, akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mhe. Ndejembi amesema, amesikiliza kwa makini taarifa ya ujenzi wa Zahanati hiyo ya Kijiji cha Mtakuja iliyowasilishwa na mratibu wa TASAF Wilaya ya Ruangwa, lakini hajaridhishwa nayo kutokana na mapungufu yaliyomo ikiwa ni pamoja na kiasi cha shilingi milioni 27 kilichoainishwa kubaki kwenye akaunti kati ya shilingi milioni 102 zilizotolewa na TASAF, hivyo hakitoweza kukamilisha ujenzi wa zahanati hiyo. 

Kutokana na mapungufu yaliyobainika kwenye taarifa hiyo, Mhe. Ndejembi amemuelekeza Kamanda wa TAKUKURU kuhakikisha anafanya uchunguzi maalum na kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.

Ni lazima tusimamie vizuri fedha za umma hususani za TASAF ambazo zinatafutwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la umaskini, na kuongeza kuwa ni lazima kuwa na uchungu na matumizi mabaya ya fedha za umma

Ndejembi 

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mhe. Hashim Komba ameunga mkono jitihada za Mhe. Ndejembi za kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha zilizotolewa na TASAF kujenga zahanati itakayoboresha huduma za afya katika Kijiji cha Mtakuja, na kuahidi kuwa kamati yake ya ulinzi na usalama itasimamia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa kamanda wa TAKUKURU ili taarifa ya uchunguzi iwasilishwe kwa wakati kwa ajili ya kuchukua hatua stahiki.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi anaendelea na ziara ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kuzinusuru Kaya Maskini, pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa umma katika Wilaya zilizopo mkoani Lindi.



Post a Comment

0 Comments