SERIKALI YAIPA JKT MITAMBO, ZANA ZA KILIMO ZA BILIONI 4

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

SERIKALI imetoa mitambo na zana za kilimo zenye thamani ya takribani bilioni 4 kwa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ili kuongeza uzalishaji wa chakula hapa nchini huku ikilipongeza Jeshi hilo kwa kuendelea kusimamia malengo ya kuanzishwa kwake na kutimiza majukumu ya malezi ya vijana na uzalishaji mali ili kujenga uchumi na Taifa kwa ujumla.

Zana hizo ambazo zimetoka nchini Italia zenye uwezo wa kulima Hekari 500 kwa siku, zitaliwezesha jeshi hilo kujilisha kwa asilimia 100 ifikapo 2025 na ziada ya chakula kutumika kama biashara ndani na nje ya nchi.

Akikabidhi zana na vifaa hivyo, Waziri wa Ulinzi  na Jeshi la Kujenga Taifa Innocent Bashungwa amesema fedha hizo ni sehemu ya bajeti ya mwaka wa fedha  katika mwaka wa fedha 2021/22 zilizotolewa na Serikali, na kuongeza tija ya uzalishaji mali hususani katika eneo la kilimo chini ya Jeshi la kujenga Taifa ili kuondokana na kilimo cha mkono na kutumia Teknolojia ya kisasa.

Nishukuru uongozi wa Jeshi la kujenga Taifa kwa maandalizi ya hafla hii fupi ya uzinduzi wa mitambo na zana hizi za kilimo ambazo zitatumika katika uzalishaji mali na kuongeza tija na ufanisi katika kilimo ndani ya jeshi la kujenga Taifa

Bashungwa

Aidha Waziri Bashungwa amesema kuwa jitihada hizo za kutumia zana za kisasa na Teknolojia ya kisasa chini ya jeshi la kujenga taifa ni sehemu ya mkakati wa kusaidia taifa na mpango mzima wa kuhakikisha zinafanya jitihada za uzalishaji ili kuweza kujitosheleza kwa chakula hapa nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Stergomena Tax amesema kuna upungufu wa utekelezaji wa miundombinu mbalimbali hususani miundombinu ya mradi wa Umwagiliaji wa Chita na Mgeta, kutokana na hilo alisema zinahitajika sh Bilioni 10 kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa mradi huo.

Kunahitajika fedha kwa ajili ya kutekeleza miundombinu ya miradi mbalimbali ikiwemo kilimo cha umwagiliaji katika maeneo ya Mgeta na Chita

Tax.


Awali akimkaribisha Mkuu wa Majeshi Mwenyekiti wa Kilimo Mkakati Mifugo na Uvuvi Brigedia Jenerali, Hassan Mabena alisema wamejipanga kuhakikisha wanafanya kilimo chenye tija ili kuhakikisha Jeshi hilo linajitosheleza kwa chakula.

Kutokana na hilo amesema wanaishukuru serikali kutokana na zana hizo ambazo wanaamini watatekeleza miradi ya kilimo kwa weledi.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Jacob Mkunda amesema JKT inapaswa kubuni na kuanzisha viwanda ili kuongeza kipato ndani ya Jeshi hilo.

Naye Mkuu wa JKT, Meja Jenerali Rajabu Mabele, ameishukuru serikali kutokana na kutoa fedha hizo za kununua zana za kilimo.

Hata hivyo kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi Dk Faraji Mnyepe amesema Wizara itaendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo ili kuhakikisha Kilimo kinasonga mbele.

 

 

Post a Comment

0 Comments