MAKUSANYO MADINI YAONGEZEKA.

📌 RHODA SIMBA

TUME ya Madini imefanikiwa kuongeza kiwango cha makusanyo ya maduhuli ya serikali kutoka sh.bilioni 346.2 mwaka 2018/2019 hadi sh.bilioni 624.61 mwaka 2021/2022 sawa na ongezeko la asilimia 44.5.

Pia, imesema mwaka 2021, mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 4.8 kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 7.3 lengo ni kuchangia ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 10 ifikapo 2025.

Hayo yamebaishwa leo Oktoba 7 Jijini hapa, na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji na vipaumbele vya taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023

Ukuaji wa sekta ya madini mwaka 2021 ulikua kwa asilimia 9.6 ukilinganisha na ukuaji wa asilimia 1.5 kwa mwaka 2018. Aidha, jumla ya mitambo mitatu ya kusafishia dhababu imejengwa na mashine 23 za kuongeza thamani madini zimekamilika

Mhandisi Samamba amesema tume imewezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kukusanya kodi mbalimbali kutoka katika migodi mikubwa ambapo kuanzia mwaka wa fedha 2019 hadi kufikia Mei, 2022 ni takriban sh. trilioni 3.77.

Amesema fedha hizo ni nje ya zile ambazo tume ilikusanya kutokana na mauzo ya bidhaa zitokanazo na madini.

Mhandisi Samamba amefafanua kuwa katika kipindi cha mwaka 2018 hadi 2021, Tume imesimamia vyema suala la usalama, afya, mazingira na matumizi ya baruti migodini kwa kushirikiana na taasisi zingine. 

Amesema katika kuhakikisha wananchi wanakuwa salama walifanikiwa kukagua migodi 141 mikubwa, kati na midogo kwa ajili ya kuangalia kama imezingatia usalama wa watu wanaofanya kazi katika maeneo hayo.

Ajira kwa wazawa katika migodi imefikia asilimia 97 ikilinganishwa na asilimia 70 iliyokuwepo mwaka 2018. Kupitia ajira hizo, watanzania wameendelea kupata ujuzi na uzoefu ili baadaye miradi hii isimamiwe na watanzania kwa asilimia 100

VIPAUMBELE VYA BAJETI YA MWAKA HUU.

Mhandisi Yahya amesema katika mwaka huu wa fedha tume ya madini imejipanga kukusanya sh. bilioni 822 kupitia maduhuli yatokanayo na shughuli za migodi.

Aidha imesema itawafutia leseni wamiliki ambao wanamiliki migodi na wameshindwa kuendeleza.

Kuendelea kufungamanisha sekta ya madini na sekta zingine, kusimamia ipasavyo ushiriki wa wazawa, kuendelea kuvutia wawekezaji, kuzuia kupambana na utoroshaji na biashara haramu ya madini na kuendelea kutoa elimu kwa umma na wawekezaji

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari - MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Tanzania imejaaliwa na Mungu kuwa na utajiri mkubwa wa madini.

Amesema kwa sasa kinachofanyika ni kutafiti kufahamu yalipo ili yaweze kunufaisha nchi, katika kutekeleza hili tunashirikiana na sekta binafsi.

Mtazamo wa Serikali kwa sasa ni kupanua wigo wa kunufaika na madini kwa sababu tumefanya utafiti wa kubaini madini yetu kwa asilimia 16 tu, hivyo tunataka tujadiliane na wadau ili kuchimba maeneo mengi zaidi

Tunataka tufanye utafiti wa kina kujua madini mengi zaidi angalau kufikia asilimia 40 ili Serikali ijenge mazingira mazuri na kuzihamasisha sekta binafsi kuchimba madini hayo.

 

 

 

 

 


Post a Comment

0 Comments