📌RHODA SIMBA
SAKATA la ndugu wa marehemu Richard Bukombe mkazi wa Miyuji jijini Dodoma aliyefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kugongwa na gari mali ya jeshi la Magereza limechukua sura mpya baada ya wanafamilia kumtaka Mkuu wa Jeshi la Magereza, kutowakingia kifua waliohusika.
Aidha, wameiomba Tume ya Haki za Binadamu pamoja na Kituo cha Haki za Binadamu na Msaada wa Kisheria (LHRC) kuingilia kati sakata hilo ili kifo cha ndugu yao kipatiwe haki.
Akizungumza na waandishi wa habari Jijini hapa kwa niaba ya familia mdogo wa marehemu Bukombe Bulole, amesema pamoja na kuzika mwili wa ndugu yao bado hawatakata tamaa ya kupata haki ya ndugu yao.
Amesema baada ya kuuzika mwili wa marehemu walifuatilia katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo ilibainika kuwa mwili wa ndugu yao uliletwa na kutelekezwa katika chumba cha kuhifadhia maiti na askari wa Jeshi la Magereza.
Kamishna anapaswa kulifanyia kazi hili kwani lipo mikononi mwake asiwape kazi viongozi wake wa juu kwa ajili ya kuwalinda wahahusika, tunamuomba sana atusaidie hakuna haja sisi kumfuata Waziri Mkuu au Rais Samia Suluhu Hassan afanye kitu ambacho ni jukumu la mteule wakeBukombe
Amesema kuendelea kukaa kimya kwa jeshi la Magereza kunazidi kuwapa hofu kuwa ndugu yao alipogongwa na gari hakuwa amekufa bali wao ndiyo waliomalizia ili kuondoa ushahidi.
Ndugu wanahabari sheria ya usalama barabarani kifungu cha 57 ii b kinamtaka mtu yeyote atakaye sababisha ajali aripoti kituo cha polisi ndani ya saa 12 ila sheria itamsamehe na endapo akichelewa atakuwa hawezi kutimiza takwa la sheria hiyo.
Lakini pia kifungu cha 40 sura ya168 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inasema kwamba mtu yeyote atakayesababisha majeruhi au kifo kwa mujibu wa sheria ya usalama barabarani atakuwa ametenda kosa la jinai
Amesema kwakuwa askari Magereza ni miongoni mwa vyombo vinavyohakikisha sheria ya nchi haivunjwi na kwa kutoripoti ajali ile kituo cha polisi wamevunja sheria.
Hivyo askari Magereza ambao ni wasimamizi wa sheria za nchi wametenda kosa la jinai na tunawaomba viongozi wao wawafikishe mahakamani mara moja bila kusumbua vyombo vingine vya usalama kuchunguza jambo hilo
Bukombe
Vilevile, alisema familia inamuomba Kamishna wa Magereza aige mfano wa Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu George Simbachawene alivyoruhusu sheria ifuate mkondo wake kwa mtoto wake ambaye alivunja sheria za nchi.
Bukombe, alisema toka ajali imetokea Septemba 13, mwaka huu hadi leo hii ni zaidi ya siku 14, zimepita bila kuona chochote kilichofanywa na Magereza zaidi ya danadana za kuvuta muda ili wasahau na kuacha kufuatilia jambo hilo.
Marehemu Richard Bukombe, maarufu kwa jina la Baba Paroko anadaiwa kugongwa na gari mali ya Jeshi la Magereza (Land cruzer pick up) Septemba 13, mwaka huu jirani na eneo la Twiga hotel Msalato jijini hapa.
Kwa mujibu wa ndugu zake wanadai aligongwa na gari hilo mali ya Magereza majira ya saa 12:30 jioni ambapo baadhi ya askari wa jeshi hilo walimchukua na kuondoka naye na baadaye mwili wake kukutwa umetelekezwa mochwari.
Mkuu wa Jeshi la Magereza Mkoa wa Dodoma Kenneth Mwambije, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alikiri kuwa analifahamu kama ambavyo watu wengine wanavyolisikia lakini akasisitiza kuwa watu wa kulitolea ufafanuzi ni makao makuu ya Jeshi hilo.
Wiki iliyopita Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Yussuf Hamad Masauni, alipoulizwa kuhusu tukio hilo alisema anaomba kwanza kukutana na wanafamilia hao ili kusikiliza malalamiko yao.
0 Comments