📌RHODA SIMBA
Wakala wa Nishati
Vijijini (REA) umeendesha Semina ya kuwajengea uwezo Wabunge Wanawake kuhusu
Mradi wa kusambaza nishati safi na salama ya kupikia vijijini.
Akifungua Semina hiyo iliyofanyika Dodoma, hivi karibuni, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mussa Azan Zungu aliwahamasisha Washiriki kuwa mfano kwa wananchi katika maeneo yao, namna gani wanaweza kupikia nishati ambayo ni salama.
Tuzingatie na tusaidiane kupeleka nishati mbadala kwenye maeneo yetu na hasa sisi wabunge, tuanze kuonesha mfano.
Aidha, amezungumzia suala la uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa ambapo amesema pamoja na mambo mengine, umeathiri Mlima Kilimanjaro ambacho ni kivutio cha utalii nchini.
Akifafanua, amesema utafiti unaonesha kuwa hewa ya moto ambayo hupaswa kupozwa na miti hususan katika mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Tanga, inakwenda kwenye Mlima Kilimanjaro jambo linalochangia kupoteza barafu yake.
Naibu Spika alisisitiza kuwa Wabunge Wanawake wana nafasi kubwa ya kuleta mabadiliko chanya kwenye eneo la nishati safi na salama na kuokoa afya za watumiaji wa kuni na mkaa hususan akina mama na watoto.
Tumeambiwa na Wataalam kuwa Mama akipika kwenye moshi kwa saa moja ni sawa na kuvuta sigara mia tatu. Kwa hali hii atakuwa ameathirika kwa kiwango kikubwa na kwa wenye ujauzito itamuathiri hata mtoto aliye tumboni.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba, akizungumza kupitia video fupi iliyorekodiwa na kuchezwa katika semina hiyo, aliomba ushirikiano kutoka kwa Wabunge Wanawake katika kufanikisha mkakati huo maalum unaotekelezwa na Wizara kupitia REA, ili kuleta mapinduzi katika nishati ya kupikia hususan vijijini.
Waziri Makamba ambaye hakuweza kushiriki katika Semina husika kutokana na majukumu mengine ya kitaifa, alibainisha kupitia video hiyo fupi kuwa athari za matumizi ya kuni na mkaa ni kubwa hasa kwa akina mama na watoto lakini hazisemwi sana kwani kundi linaloathirika zaidi halina sauti.
Akitoa takwimu, alisema kuwa utafiti unaonesha takribani watu 33,000 hupoteza maisha kila mwaka hapa nchini kutokana na kuvuta hewa ya ukaa inayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa katika kupikia.
Alisema kuwa kutokana na madhara makubwa yanayosababishwa na matumizi ya nishati zisizo salama, Wizara kupitia REA imeamua kuweka juhudi za makusudi kuhakikisha inawakomboa akina mama hususan waishio vijijini kutoka katika madhara ya kiafya pamoja na kupunguza athari kwa mazingira.
Akizungumza katika Semina hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula, alipongeza kazi kubwa iliyofanywa na REA katika kupeleka nishati ya umeme vijijini na kuongeza kuwa kazi ya kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala kwa kupikia vijijini ni kubwa zaidi hivyo Wakala unapaswa kuungwa mkono katika utekelezaji wake.
Kwahiyo Wabunge wenzangu, tulichukue jambo hili, tulisemee kwa nguvu kubwa kwa umoja wetu ili tuweze kupata matokeo chanya ambayo wote tunayatarajia
Mwakilishi wa Wizara ya Nishati katika Semina hiyo, Mhandisi Edson Ngabo alisema kuwa katika kuhakikisha upatikanaji wa nishati bora ya kupikia, Serikali imeanza utekelezaji awamu kwa awamu ambapo katika Mwaka huu wa Fedha (2022/23) Shilingi Bilioni Tano zimetengwa kwa ajili ya kusambaza gesi asilia kwa ajili ya kupikia katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.
Awali, akitoa salamu za ukaribisho, Mwenyeji wa Semina hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy, alisema kuwa, kwa kutambua kwamba kuna madhara ya kuendelea kutumia nishati isiyo salama, Serikali imekuja na Mpango Maalum wa kuwezesha upatikanaji wa nishati bora ya kupikia vijijini.
Ameeleza zaidi kuwa, katika Mpango huo, kuna maeneo kadhaa ya kipaumbele ikiwemo kujenga ufahamu, hasa kwa wananchi kuhusu upatikanaji na kuhamasisha matumizi ya bidhaa na teknolojia za nishati bora vijijini.
Mkurugenzi Mkuu alifafanua kuwa, baadhi ya watu hawafahamu kama kuna majiko hivi sasa yanayotumia kiwango cha nishati inayotumika kupikia mlo mmoja na kutumia kiwango kilekile kupikia mlo zaidi ya mmoja.
Kwahiyo, tutawajengea ufahamu kuhusu upatikanaji wake na kuhamasisha pia matumizi yake, tukiwalenga zaidi wananchi wa vijijini
Mhandisi Saidy.
Akiwasilisha Mada katika Semina hiyo, Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, ametaja baadhi ya madhara yatokanayo na matumizi ya nishati isiyo bora na salama kwa kupikia kuwa ni pamoja na kupoteza nguvu kazi ya Taifa.
Mhandisi Mwijage
alibainisha kuwa vifo vitokanavyo na uvutaji wa hewa ya ukaa majumbani ni
asilimia 8.5.
Semina hiyo kwa Wabunge Wanawake ilihudhuriwa pia na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, Wabunge Vinara, Menejimenti ya REA, Mwakilishi kutoka TPDC pamoja na Wadau mbalimbali wanaojishughulisha na uendelezaji wa teknolojia mbadala za nishati ya kupikia
0 Comments