MWANAFUNZI wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Elizabeth Massawe amebuni mashine ya 'Automatic Milk Vending' ambayo inatumia mfumo wa kidigitali kuuza maziwa na kumrahisishia mfanyabiashara kupunguza gharama za kuajiri na badala yake atakuwa anangalia kwa kutumia mfumo huo kujua wateja wangapi walionunua maziwa na amepata kiasi gani kwa siku.
Ameomba serikali kuchukua muda wa kutathimini bunifu mbalimbali zinazobuniwa na wanafunzi wa vyuo ili kuziendeleza na kuweza kutoa ajira kwa vijana wengi wa kitanzania kwa lengo la kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Akizungumza leo Septemba 22,2022, kwenye maonesho ya maadhimisho ya Siku ya wahandisi Jijini hapo katika banda la NIT, Elizabeth amesema kuwa mashine hiyo inafanya kazi kwa kutumia mfumo wa kidigitali ambapo mfanyabiashara atakaa nyumbani huku biashara yake ya maziwa inaendelea kama kawaida.
Mwanafunzi huyo ameeleza kuwa mteja atakapohitaji maziwa ataweka kiasi cha fedha na atapata maziwa kulingana na hela yake huku akitolea mfano mteja huyo akiweka shilingi 100 atapata maziwa milimita 300 na taarifa itamfikia mmiliki kupitia web site yake.
Amesema lengo la kubuni teknolojia hiyo ni kumsaidia mfanyabiashara asitumie mikono na muda mwingi kufanya biashara hiyo kama kusafisha kila dakika katika eneo lake la biashara na ukusanyaji wa hela.
Mmiliki wa hii mashine atakuwa anajaza maziwa pale yatakapokuwa yameisha na kuendelea na shughuli nyingine na atajua kupitia mfumo wateja wangapi wamenuna maziwa na kiwango cha fedha kinaonekana, tarehe na muda wa mteja alionunua maziwa
Amefafanua kuwa kupitia mashine hiyo mmiliki atajua ameuza kiasi gani na wateja wangapi waliofika kununua maziwa na glasi ngapi kwa siku ameuza.
Elizabeth amesema hadi kukamilika kutengeneza mashine hiyo imechukua muda wa miezi miwili na gharama za malighafi ni shilingi 180,000.
Akizungumzia changamoto katika utengeneza wa mashine hiyo Elizabeth amesema kuungua kwa vifaa mara kwa mara hali iliyomsababishia kufikisha muda huo.
Akizungumzia teknolojia hiyo Mkazi wa Makulu aliyetembelea banda hilo Jonathan Alex ameitaka jamii kuondoa dhana ya kwamba mwanamke hawezi kufanya jambo kubwa ambalo linaweza kufanywa na mwanaume.
0 Comments