DC SHEKIMWERI AWATAKA TAKUKURU KUWA NA SEMINA ZA UELEWA KWA WATUMISHI WA UMMA

 

📌RHODA SIMBA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini TAKUKURU imeshauriwa kuwa na vikao kazi na semina ili kuwajengea uelewa watumishi wa Umma hasa katika maeneo ya manunuzi ili miradi inayofanyika iendane na thamani halisi ya fedha ili kuondokana na rushwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Jijini Dodoma na Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini,Jabir Shekimweri alipotembelea Mabanda mbalimbali kwenye wiki ya maonesho ya maadhimisho ya Miaka 20 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora yanayofanyika katika viwanja vya Jakaya Kikwete ambapo Taasisi mbalimbali za Msaada wa Sheria zimeshiriki.

Lazima tukili kwamba kuna changamoto kwenye sehemu ya rushwa, vitu viwili naendelea kusisitiza cha kwanza kumlea samaki akiwa mchanga, wanafanya kazi nzuri na mimi kwenye Wilaya nimeandaa midahalo tunashindanisha shule kwenye kupinga masuala ya rushwa kwa njia ya mdahalo

Tunawakutanisha wanafunzi wanafanya midahalo tunawajenga wakiwa wadogo ili wanapokuwa wajue nchi yao inatakiwa kuwaje

Shekimweri

Aidha Shekimweri amewataka wananchi kujitokeza kwenda kupata elimu juu ya haki mbalimbali ambazo zinatolewa katika viwanja vya Jakaya Kikwete.

Nae Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora, Jaji mstaafu Mathew Mwaimu amesema kuwa kama Tume wamekuwa wakipokea malalamiko mbalimbali yakiwemo ya migogoro ya ardhi, Jeshi la polisi kulalamikiwa kubambikiza kesi pamoja na kutesa wananchi ikiwemo na masuala ya rushwa.

Nyakati hizi naona malalamiko ya migogoro ya ardhi yanayoletwa si mengi sana lakini yale machache yanayotufikia tumeyashughulikia kwa kufanya chunguzi na kutoa mapendekezo kwa taasisi husika na kuyachukulia hatua.

 


Kuhusu masuala ya unyanyasaji haya mara nyingi yakija kwetu kule polisi kuna dawati, tunayapeleka dawati la jinsia na wao wenzetu wanaanzisha mchakato wa upepelezi” amesema Jaji Mwaimu

Maadhimisho hayo yanaenda sambamba na kaulimbiu isemayo "Miaka 20 ya kuhamasisha ulinzi wa hifadhi ya Haki za binadamu na misingi ya utawala bora".

 

Post a Comment

0 Comments