WIZARA YA AFYA YAWATAKA WANANCHI KUKAMILISHA DOZI YA UVIKO 19

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

WAKATI takwimu zikionesha kuwa bado kuna idadi kubwa ya watu wasio kamilisha dozi ya Uviko 19, Wizara ya Afya imewataka kufanya hivyo ili kuzuia kupata ugonjwa mkali unaoweza kusababisha kifo pale mtu anapoambukizwa.

Takwimu za Wizara ya Afya zinaonesha watu laki 775,398 waliotakiwa kukamilisha dozi ya pili ya Sinopharm na Pfizer Julai 31 mwaka huu, hawakukamilisha.

Pia takwimu za Wizara hiyo zinaonesha watu laki 872,821 waliotakiwa kurudi kukamilisha dozi hizo Agosti 14, hawakufanya hivyo.

Kutokana na hali hiyo, Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt Aifelo Sichalwe amewataka wananchi kukamilisha dozi za Uviko 19 ili kuongeza kinga.

Katika taarifa yake kuhusu mwenendo wa Uviko 19 kwa kipindi cha Julai 2 hadi 29 mwaka huu, Dkt Sichalwe alisema wananchi waliopata dozi kamili ni 4,223,670.

Amesema idadi hiyo ni ongezeko la watu 1,182,519 ikilinganishwa na kiwango cha uchanjaji katika mwezi mmoja uliopita ambapo watu 3,041,151 walipata chanjo.

Wizara inatoa tahadhari kwa wananchi wote kuendelea kuchukua hatua za kujikinga na Uviko 19 ikiwa ni pamoja na kupata kwa wakati dozi kamili za chanjo ya ugonjwa huu

Dkt Sichalwe.

Aidha taarifa hiyo imeonesha kuwepo kwa visa vipya 543 vilivyothibitika kuwa na maambukizi mapya ikilinganishwa na 352 kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita ikiwa ni ongezeko la asilimia 54.3.

Katika kipindi hicho hakuna kifo kilichotokea, jumla ya wagonjwa 10 walilazwa na wote hawajapata chanjo

Dkt Sichalwe 

Aidha takwimu zinaonesha watu waliothibitisha kuwa na ugonjwa huo walitoka katika mikoa 13 nchini ikiongozwa na Dar es Salaam (366), Mwanza (41), Mbeya (24), Shinyanga (20), Katavi (19), Arusha (16) na Lindi ni 13.

Mikoa mingine ni Kilimanjaro (12), Mtwara (12), Mara (7), Simiyu (5), Tabora (2), Kagera (2), Morogoro (2), Iringa (1) na Dodoma (1).

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa wiki ya Julai 23 hadi 29, idadi ya visa vipya imeongezeka kwa asilimia 52 Pasifiki ya Magharibi, asilimia 45 kwa Mediterania Mashariki na asilimia 13 kwa Kusini Mashariki kwa Asia.

Mtaalamu wa Masuala ya Uelimishaji wa Umma kuhusu Kovid 19, kutoka Wizara ya Afya, Juliana Mshama amesema lengo la Serikali ni kufikia asilimia 70 ya watanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea wawe wamepata chanjo ya Uviko 19 hadi kufikia Disemba, 2022.

Akitoa mada kwenye mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu Uviko 19, Jijini Dodoma, Mshama amesisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo.

Ametaja njia za kujikinga na maambukizi hayo kuwa ni kuvaa barakoa wanapojisikia dalili za mafua na kwenye mikusanyiko kuzuia kusambaa kwa maambukizi, kuzingatia usafi hasa kunawa mikono, kufanya mazoezi, kula vyakula bora na kutoa taarifa za kuwepo watu wenye dalili hizo

 

 

 

 

Post a Comment

0 Comments