📌RHODA SIMBA
WAKULIMA mkoani Dodoma hasa wanaojihusisha na kilimo cha zao la Zabibu wamesisitizwa kutumia fursa zinazopatikana kwenye mtandao kupata taarifa sahihi zitakazowezesha kuongeza tija katika shughuli za uzalishaji wa kilimo, sambamba na kupata fursa na taarifa za masoko.
Akizungumza katika banda la maonyesho la Mamlaka hiyo kwenye maonesho ya kilimo mkoa wa Dodoma Meneja TCRA Kanda ya Kati Boniface Shoo amesisitiza kuwa elimu ya kutosha inayowezesha ukuzaji tija katika shughuli za kilimo katika zama za sasa inapatikana kwenye mtandao.
Katika anga la mtandao tunazo fursa nyingi sana zinazowezesha wakulima hasa wakulima wa mkoa wetu wa Dodoma wanaojishughulisha na kilimo cha Zabibu kupata elimu ya kila namna kuhusu kilimo bora; TCRA tunawasisitiza wakulima kutembelea majukwaa ya kimtandao kupata elimu hii muhimu. Pia kubwa zaidi ni kupata mwanga wa mwenendo wa masoko ya bidhaa za mazao yao hasa Zabibu
Shoo.
Kwa upande wake Afisa Mawasiliano wa TCRA Makao Makuu Bw Robin Ulikaye amewaasa wananchi kuwa makini na utapeli unaoendelea mitandaoni na kutoa taarifa za utapeli huo
Mtumiaji wa huduma za Mawasiliano ya simu mara anapopokea ujumbe wa kitapeli au kupigiwa simu ya kitapeli kwenye mtandao wake wa mawasiliano, tunamshauri atoe taarifa juu ya utapeli huo kwa kutuma neno ‘utapeli’ kwenda namba 15040 kisha atapokea ujumbe unaomtaka kuwasilisha namba iliyomtumia ujumbe wa kitapeli; awasilishe namba hiyo na kikosi-kazi maalum kitapokea taarifa hiyo na kuifanyia kazi
Ulikaye.
Afisa huyo amesisitiza kuwa kutoa taarifa za utapeli hasa kwa jumbe za “ile pesa tuma kwenye namba hii…” kunasaidia kupunguza matukio ya utapeli mtandaoni.
Pia tunawaomba wananchi wanaotumia huduma za Mawasiliano ya simu wahakikishe wanahakiki namba zao za simu zilizosajiliwa kwa namba za Kitambulisho cha Taifa ili wasalie kuwa salama wakati wote wanapotumia Mawasiliano; uhakiki wa laini za simu zilizosajiliwa kwa kitambulisho chako ni muhimu kwani unaepusha utambulisho wako kutumiwa na mtu mwingine, hasa isivyo halali” amebainisha na kuongeza.
TCRA ilibainisha kuwa zoezi la uhakiki wa Mawasiliano linakamilika kwa kubofya alama ya nyota Mia Moja na Sita kisha alama ya reli (*106#) ambapo mtumiaji atafuata maelekezo na ikiwa kuna namba asizozitambua au kuzihitaji anaweza kuzifuta kwa usaidizi wa mtoa huduma wake wa Mawasiliano.
Kuhusu udhalilishaji mtandaoni Mamlaka hiyo ilisisitiza kuwa mtu yeyote anapotendewa udhalilishaji kwenye mtandao anapaswa kutoa taarifa kwa mamlaka husika ambayo ni Jeshi la Polisi ili hatua stahiki za Kisheria ziweze kuchukuliwa.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ni taasisi ya Serikali yenye jukumu la kusimamia sekta za Mawasiliano na Utangazaji Tanzania. Ilianzishwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania Na. 12 ya mwaka 2003 kusimamia huduma za kielektroniki na posta na masafa ya mawasiliano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mamlaka ilianza kazi tarehe 1 Novemba 2003 na inafanya shughuli za zilizokuwa Tume ya Mawasiliano Tanzania (TCC) na Tume ya Utangazaji Tanzania (TBC).
0 Comments