📌JASMINE SHAMWEPU
WACHIMBAJI wadogo wa madini ya dhahabu nchini
wameshauriwa kujiunga na kuwekeza kwenye mitambo ya kisasa ya uzalishaji na
uvunaji wa dhahabu yenye tija kutokana na ugunduzi wa teknolojia yenye uwezo
mkubwa wa uzalishaji ambao ni rafiki kwa mazingira.
Mtambo huo aina ya CIP unakadiriwa kuwa na
thamani ya shilingi milioni 100 na kwamba unaweza kutumika kuchenjua madini ya
dhahabu kwa muda mfupi na gharama nafuu bila kuwa na athari za kiafya kwa
binadamu kama ilivyo kwa matumizi hatari ya zebaki.
Akizungumza na Timu ya watalaam kutoka Sekta
ya Madini, wajumbe kutoka Baraza la Kuhifadhi Mazingira, (NEMC) na wachimbaji
wadogo wanaofanya ziara Mkoani Mwanza, Meneja Mradi wa eneo la Mgodi wa
Kiwanga Dynast Plant, John Mashalla, amesema kuvuna madini kwa kutumia mtambo
huo, ni chachu ya uvunaji mzuri wa dhahabu, kwa kuwa ni mfumo mzuri unaotumika
kuhifadhi mazingira na viumbe hai wengine wa asili ambao walikuwa hatarini
kupotea kutokana na matumizi ya zebaki.
Mfumo huu unasaidia katika uvunaji wa dhahabu, kuvuna zaidi na hata kubakiza kwenye udongo kiwango cha asilimia 0.03 ya madini hayo kutokana na ubora wake na manufaa makubwa zaidi,” alifafanua na kuongeza kuwa mtambo huo unasaidia wachimbaji wadogo kujiepusha na matumizi ya zebaki ambayo inasadikiwa kuenea katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kwa kutumia mtambo wa CIP, mawe yaliyopondwa na kuwa udongo huingizwa kwenye mfumo ambao haujapitishwa kwenye zebaki na kufanya uvunaji dhahabu kufanyika bila uharibifu na uchafuzi wa mazingira,” alisema Mashalla.
Amehimiza wachimbaji wadogo kutembelea eneo la
mradi huo ili kujifunza na ikiwezekana wajiunge na kumiliki au kuendesha mtambo
wa aina hiyo ili kuingiza kipato kikubwa na wakati huo huo kujiepusha na
madhara ya zebaki ambayo inasadikiwa kuwa chanzo kimojawapo cha kueneza magonjwa
aina ya saratani hasa kwenye ukanda wa Ziwa Nyanza.
Kwa ubora na mafanikio ya uzalishaji wa dhahabu majaribio ya awali yameonesha faida kubwa ya matumizi ya mtambo huo kwa kuwezesha wachimbaji kujiepusha na matumizi ya zebaki ambayo ni hatari, kuingiza udongo unaotokana na mawe na kuepuka uharibifu wa mazingira.
Kituo cha mfano cha uchenjuaji wa dhahabu kata ya Lwamgasa mkoa Geita kwa ajili ya kudhibiti matumizi ya Zebaki na kuelekeza njia sahihi za uchenjuaji wa dhahabu. |
Naye Afisa madini kutokaTaasisi ya Jeolojia na utafiti wa madini Dodoma, John Shija amesema Serikali kwa muda mrefu imekuwa mstari wa mbele kutafuta njia mbadala ya kuepusha wachimbaji wadogo dhidi ya matumizi ya Zebaki na kwamba upatikanaji wa mtambo huo utasaidia kupunguza gharama, hatari za kiafya na kuwezesha wachimbaji wadogo kujipatia fedha za kuendesha shughuli za kuchenjua dhahabu na kuvuna madini safi yenye ubora wa kimataifa.
Kwa upande wake Afisa uwezeshaji wa Matumizi
Mbadala ya Zebaki, Mhandisi Boniphace Guni, amezungumzia uwezo wa mtambo huo wa
uchenjuaji dhahabu na kufafanua kuwa teknolojia hiyo inazalishwa hapa nchini
kupitia Shirika la viwanda vidogo (SIDO) na kwamba kwa kutumia wazalishaji
wazawa, wachimbaji wa dhahabu watajiepusha na madhara ya matumizi ya Zebaki na
kuboresha uzalishaji wa madini hayo hapa nchini.
Madhara ya zebaki ni pamoja na kusababisha
magonjwa ya saratani kwa kuingia katika mfumo wa ukuaji hasa kwa watoto
kuathirika katika ukuaji wa ubongo.
Afisa kutoka tume ya madini mkoa wa Mwanza, Wilson Rwegasira, amesema Idara yake kwa ushirikiano na NEMC wamekuwa walezi kwa wachimbaji wadogo na kutoa elimu ya kuhifadhi mazingira, kuwapa mbinu za kutumia njia mbadala ya kuvuna dhahabu na kuwahamasisha kuhama kutoka matumizi ya zebaki,
Mtambo huu ni Rafiki kwa kimazingira, utasaidia kuongeza uzalishaji mkubwa bila kuharibu na kuchafua mazingira.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani madhara
ya zebaki huchukua muda mrefu hasa kwa akinamama na wasichana wakati wa umri
mkubwa na kusababisha kushindwa kuona na madhara mengine yanayoeneza saratani.
0 Comments