MKUU wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewataka wananchi kuandaa taarifa za kaya ili kurahisisha zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu.
Taarifa hizo ni pamoja na umri wa wanakaya, hali ya ajira, Elimu, taarifa za Kilimo na mifugo namba za kitambulisho cha taifa (NIDA) na namba ya simu ya wanakaya.
Akizungumza na wandishi wa habari leo jijini Dodoma Senyamule amesema maandalizi ya sensa yamekamilika kwa asilimia 98 ikiwemo mafunzo kwa makarani, vifaa vya sensa, usafiri na masuala ya kifedha kwa ajili ya kuwezesha zoezi la sensa kufanyika.
Hadi sasa makarani wamesambaa katika maeneo yao waliyopangiwa kwa ajili ya kujitambulisha kwa viongozi wa maeneo hayo kutambua eneo lake la kuhesabu watu ambapo Mkoa wa Dodoma una jumla ya makarani 10,353 ambao watafanya kazi ya kuhesabu katika maeneo waliyopangiwa
Serikali inawaomba wananchi wote kushiriki zoezi la sensa kuanzia siku ya jumanne kwa kuhakikisha wanashiriki kuhesabiwa na wanahesabiwa mara moja tu na wanatakiwa kutambua kuwa ni kosa kisheria kukataa kushiriki zoezi hilo.
Senyamule amesema katika kuhakikisha zoezi la sensa linafanyika kwa ufasaha Mkoa wa Dodoma umezindua namba maalumu ya simu ambayo kaya yoyote ambayo haitafikiwa na karani kuhesabiwa mwananchi atapiga namba hiyo bure.
Amesema mwananchi atapiga simu hiyo na kueleza mtaa au kitongoji anapoishi na uongozi wa Mkoa utawasiliana na karani aliyepangiwa katika eneo hilo na kufika kuhesabu kaya husika.
Amewataka makarani kuhesabu watu katika eneo lake alilopangiwa kwa ufasaha na kutunza siri za kaya alizohoji na kutambua kazi hiyo inafanyikia kwa maslahi ya taifa katika kupanga mipango ya maendeleo.
Nitumie fursa hii kuwasisitiza wakuu wa Wilaya wote wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanasimamia zoezi hilo Ili lifanyike kwa mafanikio kama ilivyopangwa
0 Comments