NHC :TUTATUMIA BILLION 413.7 KUTEKELEZA MIRADI NA MPANGO WA UJENZI WA NYUMBA 5000.

 

📌RHODA SIMBA

SHIRIKA la nyumba la Taifa NHC limesema katika mwaka wa fedha 2022/2023 litatumia shilingi bilioni 413.7 katika kutekeleza miradi mbalimbali kama vile kutekeleza Mpango wa ujenzi wa nyumba 5000 za gharama ya kati na chini ujulikanao Samia Housing Scheme (SHS), Kukamilisha ujenzi wa mradi wa Morocco square na utekelezaji wa Sera ya ubia itakayoruhusu sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya Shirika.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Meneja habari na uhusiano kutoka shirika la nyumba la taifa NHC Muungano Saguya wakati akielezea utekelezaji wa shughuli za shirika hilo na muelekeo wa utekelezaji kwa mwaka wa fedha 2022/2023 ambapo amesema miradi mingine ni pamoja na ujenzi wa majengo ya biashara katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama, Morogoro, Masasi na Lindi.

Mradi huu wa nyumba za kuuza na kupangisha unakusudia kuenzi kazi nzuri anazofanya mheshimiwa Rais na tunatamani watanzania waje wamkumbuke kwa miaka mingi ijayo,

Asilimia 50 ya nyumba hizi zitajengwa Dar es Salaam, Dodoma asilimia 20 na mikoa mingine asilimia 30 na nyumba hizi zitaanza kujengwa mwezi Septemba eneo la Kawe Dar es Salaam (nyumba 500) na Medeli Jijini Dodoma (nyumba 100) na mradi huu utatekelezwa kwa awamu utagharimu takriban shilingi bilioni 466 sawa na dola za kimarekani milioni 200

Saguya.

Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi wa ujenzi wa nyumba amesema miradi hiyo itatoa ajira kwa watanzania zipatazo elfu ishirini na sita ana mia nne (26,400) kukuza mapato ya serikali na kukuza sekta ya fedha kupitia mikopo ya nyumba watengenezaji, wauzaji na wakandarasi pamoja na kuongeza maisha bora kwa wananchi.

Mradi wa SHS wa nyumba 5000 pekee unatarajiwa kutoa ajira zipatazo 26,400(ajira za moja kwa moja 17,600 na zisizo za moja kwa moja 8,800) pamoja na kudumisha amani na utangamano, kupunguza uhalifu mijini na kuongeza maisha bora kwa wananchi

Aidha taarifa ya UN Habitat ya hali ya idadi ya watu, inasema kuwa asilimia 50 ya watu waliishi mijini mwaka 2020 na ifikapo 2050 idadi ya watakaokuwa wakiishi mijini itafikia asilimia 70. Tanzania itakuwa na watu 135m na mwaka 2100 itakuwa na watu 286m na kuwa nchi ya 9 duniani. Hii inahitaji mipango madhubuti ya kupanga miji na upatikanaji wa nyumba

Aidha Saguya amesema shirika linadai wadaiwa sugu kiasi cha shilingi Bilion 26 ambapo kati ya hizo billion 6 zitafutwa kutokana na baadhi ya wadaiwa kufariki,na makampuni mengine kutokuendelea kufanya kazi.

Tunatoa wito kwa wapangaji na wadaiwa sugu wa kodi ya pango kuhakikisha wanalipa kodi na malimbikizo wanayodaiwa kwa kuwa Shirika kuanzia sasa linajiandaa kukusanya kodi hii kwa asilimia 100

Saguya

Ikumbukwe kuwa Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa mwaka 1962 kwa sheria Na.45 likiwa na jukumu la kuwezesha ujenzi wa nyumba na majengo mengine kwa matumizi mbalimbali hususani makazi, Ofisi na biashara kwa kuzingatia Mpango Mkakati wa Shirika wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25) ambao unalenga kusukuma mbele ujenzi wa nyumba zipatazo 10,000.

 

 

Post a Comment

0 Comments