📌RHODA SIMBA
LICHA ya Serikali kuendelea kuboresha na kuweka sera, pamoja na mikakati ya miundombinu rafiki kwa watu wenye ulemavu, lakini bado kuna changamoto ya miundombinu na hali hiyo huwafanya baadhi ya watoto wenye ulemavu kushindwa kumudu mazingira ya shule.
Aidha kutokana na changamoto hiyo inawasukuma baadhi ya wazazi wa watoto wenye ulemavu kushindwa kuwaandikisha darasa la awali.
Sera ya Taifa ya Maendeleo na huduma kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 kipengele cha 1.2.5 kinasema bado mfumo wa elimu nchini hautoi fursa na nafasi sawa kwa watoto wenye ulemavu wa aina mbalimbali.
Aidha mafunzo ya walimu na mitaala ya shule kadhalika haizingatii mahitaji maalumu ya watu wenye ulemavu, kwa mfano matumizi ya lugha ya alama na maandishi ya nukta nundu.
Kutokana na mazingira haya idadi ya watoto wenye ulemavu wanaoandikishwa darasa la kwanza ni chini ya asilimia moja na idadi ni ndogo zaidi katika shule za sekondari na vyuo.
HALI ZILIVYO KWENYE BAADHI YA SHULE.
Michael Mfanyakazi ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Viwandani iliyopo hapa mkoani Dodoma,ambae yeye ana ulemavu wa viungo. Anasema changamoto anayokabiliana nayo shuleni ni maliwato.
“Hali ya vyoo vyetu hapa shuleni siyo rafiki kwangu, napata tabu sana wakati wa kwenda maliwatoni, vyoo vichache na havijatuzingatia sisi wenye ulemavu, kuna wakati najitahidi kujibana mpaka muda wa kurudi nyumbani. Naamini Serikali yetu ni sikivu naiomba ituangalie katika hili wanapotuboreshea madarasa sisi wanafaunzi wenye ulemavu wa viungo itujali na masuala ya vyoo,” anasema Mwanafunzi Michael
Wakati huo huo Trivol Ruge mwanafunzi wa kidato cha kwanza Viwandani Sekondari ambae ana uoni hafifu anasema changamoto ambayo anakutana nayo ni kutoona vizuri ubaoni.
“Nakuwa sioni vizuri ubaoni utakuta mwalimu anaandika, anafuta, mimi nakuwa sijamaliza kuandika kwa sababu natumia muda mwingi kuunganisha herufi ili niandike. Naiomba Serikali miundombinu hii iwe jumuishi kwetu sisi wanafunzi wote wenye mahitaji maalum wa aina tofauti,” anasema mwanafunzi Trivol.
Rafael Olaf ni mwanafunzi wa kidato cha pili mwenye ulemavu wa ngozi (albinism) kutoka shule ya Umonga Sekondari pamoja na Seif Mazika mwanafunzi mwenye ulemavu wa mguu wa kidato cha nne shule hiyo hiyo pia, wanaendelea kupaza sauti zao kuiomba Serikali iendele na juhudi za ukarabati wa miundombinu ya vyoo shuleni ili iwe rafiki kwao.
Shule ya Sekondari ya Patandi ni moja ya shule chache ambazo miundombinu yake imeboreshwa na kuwa rafiki kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu. |
WALIMU WAZUNGUMZA
Gerad Kailembo ni Mkuu wa idara ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule ya Sekondari Dodoma, ambapo anasema shuleni hapo wana wanafunzi wenye mahitaji maalum 71 wakiwa wamegawanyika katika vipengele mbalimbali ambapo kuna wenye ulemavu wa miguu, ulemavu wa mkono, wenye uoni hafifu pamoja na wasiosikia (Viziwi).
Akizungumzia hali ya miundombinu kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo anasema wanakutana na changamoto mbalimbali ikiwemo miundo mbinu ya vyoo, ambapo anasema idadi ya vyoo vilivyopo na wanafunzi havitoshi lakini pia havijazingatia mazingira rafiki ya wanafunzi wenye ulemavu ambapo anaiomba Serikali iongeze jitihada katika suala la ujenzi wa vyoo na kupeleka vitendea kazi kwaajili ya walimu wenye uoni hafifu.
“Wanafunzi walio wengi ni zaidi ya wanafunzi 60 wenye uoni hafifu ubaoni, na wanakutana na changamoto za kutoona maandishi yakiwa ubaoni tatizo hili limekuwa changamoto kwetu na tunalitatua wakati wa mitihani tunachapa maandishi makubwa, na tunawaweka mbele ili waone vizuri, pia tunawanafunzi ambao hawasikii vizuri lakini tumewaomba walimu waongee nao vizuri kwa kurudia rudia na inatulazimu wanafunzi hawa kuwafundisha mmoja mmoja ofisini,” anasema Mwalimu Kailembo.
Nae mwalimu Ester Simchimba Mkuu wa shule ya Viwandani Sekondari anasema ana wanafunzi wawili wenye ulemavu hali ya miundombinu katika shule ya viwandani inaridhisha kiasi si kama zamani na kutokana na juhudi za Serikali hasa katika kutambua wanafunzi wenye ulemavu madarasa yaliyojengwa hivi karibuni yamezingatia miundombinu ya wamafunzi wenye ulemavu.
“Zamani miundombinu ilikuwa si rafiki ilikuwa haimuwezeshi hata mwanafunzi ambae anatambaa kufika darasani hapa shuleni tunao wanafunzi wawili lakini tunaishukuru Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika haya madarasa ya UVIKO yamezingatia miundombinu kwa hali ya juu na kilichosalia hapa ni ukarabati yale madarasa ya zamani,
“Lakini wito wangu kwa Serikali yetu inapoboresha miundombinu yetu ya madarasa pia ituangalie na katika suala la vyoo viboreshwe kwa kuzingatia idadi ya wanafunzi na ikiwajumuisha na hawa wanafunzi wenye mahitaji maalum,”anasema mwalimu Simchimba.
Leticia Singo ni Mkuu wa shule ya Umonga Sekondari anasema shuleni hapo ana wanafunzi wanne wenye changamoto ya ulemavu na wote ni wavulana .
Akiongelea hali ya miundombinu shuleni hapo anasema miundo mbinu ni rafiki ukilinganisha na idadi pamoja na aina ya ulemavu wa wanafunzi alionao
.
Kwa kipindi cha nyuma sikuwa na madarasa ambayo ni rafiki kwa watoto nashukuru ukarabati wa mwaka jana, lakini na madarasa ya UVIKO pia yametusaidia
Mwalimu Singo.
Akitoa wito kwa Serikali, Mwalimu Singo anasema Serikali ione namna ya kuboresha miundombinu ya madarasa ya zamani ambayo hayakuwa na miundombinu rafiki kwa watoto wenye ulemavu wa miguu watoto wanapata changamoto ya kuingia darasani na kuongeza kuwa wakiwezesha fedha wakuu wa shule kupitia kamati zao za ujenzi watoe fursa ya kutumia hizo fedha kwaajili ya kuboresha miundombinu ambayo kwa sasa si rafiki kwa wanafunzi.
HAKI ELIMU.
Shule ya Sekondari Patandi ni moja ya shule zinazotoa elimu jumuishi ambako Wanafunzi wenye mahitaji Maalum wanasoma na wanasoma darasa moja na wanafunzi wasio na mahitaji maalumu. |
Godfrey Boniventura Mkuu wa miradi kutoka Shirika la HAKI ELIMU linalo jishughulisha na masuala ya utetezi wa kisera na kuhakikisha kwamba watoto wote wa kitanzania wanapata fursa ya kuwa shuleni na kupata elimu bora amesema moja kati ya eneo ambalo wanalifanyia kazi kwa sasa ni pamoja na eneo la Elimu Jumuishi (Inclusive Education).
“Elimu ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa sisi HAKI ELIMU mchango wetu umekuwa hasa kwenye matukio ya huu mkakati wa Elimu Jumuishi ambao umezinduliwa mwaka huu 2022, umebainisha namna unavyokwenda kubadilisha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi wenye mahitaji,’’
Anasema kwenye uboreshaji wa elimu jumuishi uliozinduliwa mwaka huu ulitumia mawazo na nyaraka kutoka shirika hilo limekuwa ni sehemeu ya kuboresha mkakati huo
Anaeleza kuwa mkakati wa Elimu jumuishi uliozinduliwa mwaka huu 2022 shirika limechangia mawazo na nyaraka mbalimbali za shirika hilo zimetumika kuboresha mkakati huo na Serikali imeahidi kuhakikisha kwamba mpango huo unatekelezwa.
Anaongeza kusema sekta ya elimu kwa sasa ina mpango mama ambao unaitwa( Education self development plan) wa miaka mitano na mpango huo ndio unahuisha mikakati ya makundi yote ikiwemo Elimu Jumuishi.
“Mpango huu wa miaka mitano ndio unahusisha makundi yote ambayo yemeanza utekelezaji wake kwa mwaka 2021/ 2022 na umelitambua eneo la Elimu Jumuishi kama eneo husika na limepewa eneo mahususi ambalo linazungumzia elimu ya msingi, ndani yake wakisema kuongeza udahili ubora wana eneo la tatu wanaliita Elimu Jumuishi kwenye elimu ya msingi,elimu ya sekondari,vyuo vya kati na vyuo vikuu,
“Niseme tu kwamba mpango mkakati huu umeweza kulitambua kwa mapana na umebainisha kwa namna gani wanaweza kubadilisha mazingira ya kujifunzia kwa watoto wenye mahitaji maalum” anasema Boniventura
AFISA ELIMU.
Upendo Rweyemamu ni Afisa Elimu Sekondari jiji la Dodoma anasema Serikali imekuwa ikikarabati miundombinu yake kwa wanafunzi wote mwaka hadi mwaka ili kukidhi mahitaji ya watoto wote wa kawaida na maalum.
“Zamani miundombinu ilikuwa ikijengwa ya kawaida lakini baada ya kugundua hilo tatizo kuanzia mwaka 2017 kuna mabadiliko mengi yanafanyika hasa katika miundombinu mipya ambayo inajengwa mfano kwa mwaka 2021 2022 tulitenga billion 3 kutoka mapato ya ndani kwaajili ya kujenga miundombinu mbalimbali kama madarasa maabara hostels nyumba za walimu na miundo mbinu mingine”
“Kwa upande wa Dodoma jiji ina jumla ya wanafunzi wa sekondari elfu 34,500 ambao ni jumla ya shule za Serikali na binafsi ambapo kwa shule za Serikali wanafunzi jumla wapo elfu 32 napenda kusema kwamba miundombinu yote iliyojengwa na inayojengwa kwa sasa imezingatia mahitaji ya wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa maana ya ngazi zao za kupandia darasani”anaeleza mwalimu Rweyemamu
Rweyemamu anasema jiji la Dodoma kwa idara ya sekondari ilipokea bilioni 2 na milioni 860 kwaajili ya kujenga madarasa 143 na katika shule zote zilizojengwa hayo madarasa miundombinu ya madarasa hayo imezingatia mahitaji ya watoto maalum
“Kwa mwaka 2022/2023 tumetenga kupitia mapato ya ndani billion 1 na million 600 ili kuweza kuendeleza miundombinu hii ikiwa ni pamoja na maabara vyumba vya madarasa na miundombinu mingine .
“Lakini pia kuna milion 400 kutoka Serikali kuu tumezibajetia ambazo zitakuwa na ujenzi wa hostel bwalo pamoja na maabara wataalam wetu ambao ni wahandisi wetu wanazingatia miundombinu.”anasema Mwalimu Rweyemamu
0 Comments