MAUZO YA BIDHAA YA NDIZI NA VIAZI YAPUNGUA SOKO LA MAJENGO, DODOMA.

📌AGNESS PETER

KUFUATIA kufungwa kwa shule na vyuo nchini baadhi ya wafanyabiashara kutoka soko la majengo Jijini Dodoma wamesema hali ya biashara ni ngumu kwa sasa hasa kwa bidhaa kama viazi na ndizi kutokana na uhaba wa wateja ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi.

Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na wafanyabiashara wa ndizi na viazi kutoka soko la majengo Kaiza Wiliam ambapo amesema wanategemea mzunguko wa wanafunzi katika kufanya biashara lakini kwa sasa hali imekuwa ngumu kutokana na likizo.

Amesema licha ya bidhaa ya ndizi kuwa ndio msimu wake kwasasa lakini bei yake imepanda kutokana na nauli ya kutoa shambani kuongezeka hivyo hata wateja wamepungua kwa kiasi kikubwa.

Zamani tulikuwa tunasafirisha mkungu mmoja kwa shilingi 5000 lakini kwa sasa imepanda nauli ya mkungu mmoja ni sh.8000 hadi 9000 kuna wakati tulikuwa tunakuja na magari ya mizigo mpaka majengo ila kwasasa tunafata Ndugai ukiangalia na wanafunzi wamefunga basi hali ya biashara inakuwa ngumu na wateja hakuna

Aidha Prisca John ambae ni mfanyabiashara katika soko hilo amesema kwa wastani wiki moja walikuwa wakishusha maroli ya viazi manne hadi matano lakini kwa sasa imepungua hadi maroli mawili kutokana na wateja wakubwa ambao ni wanavyuo na wanafunzi kupungua.

Amesema wafanyabiashara wa soko hilo wanapata changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na ugumu wa usafirishaji kwa kufaulisha kutoka bidhaa inakotoka hadi kufika sokoni kwaajili ya kuuzwa.

Roli likitoka Mbeya na mzigo linafikia soko la Ndugai tunafaulisha kwenye kirikuu au kenta ndogo hadi kufika soko la majengo kwahiyo gari la viazi kwa hapahapa mjini linapoteza hadi laki 3 na ndizi laki 4 kwasababu ya kufaulisha kwahiyo hata faida kwasasa hakuna.

Kwa upande wake Daudi Cosmas amesema kwasasa wanafanya biashara kwa kutumia uzoefu wa kazi lakini mzunguko wa biashara hauridhishi kutokana na walaji wengi kupungua hasa kwa chakula kama chipsi kinachopendwa na wanafunzi.

Biashara ya Ndizi na Viazi ni miongoni mwa biashara ambayo imesaidia baadhi ya vijana kujikwamua kiuchumi kwa kufanya biashara ya kuuza chakula aina ya chipsi.  



Post a Comment

0 Comments