MADHARA YA ZEBAKI CHANGAMOTO KWA WACHIMBAJI WADOGO WA DHAHABU


📌JASMINE SHAMWEPU.

MATUMIZI ya Zebaki yalianzia nchi zilizoendelea miaka mingi iliyopita ikiwa njia pekee ya awali ya uzalishaji wa dhahabu iliyotumiwa na wachimbaji wadogo na wakubwa. Hata hivyo madhara ya kemikali hiyo katika mazingira na afya ya binadamu yalisukuma watafiti kuja na njia mbadala ambazo zinaondoa zebaki na kupanua uzalishaji wa dhahabu kwa wingi na kwa muda mfupi bila madhara. Mwandishi wetu Jasmine Shamwepu aliyeungana na timu ya wataalam wa mazingira kwenye ziara ya mafunzo mkoani Mwanza na Geita anasimulia madhara ya zebaki na mbinu mbadala za kutunza mazingira na afya bila kutumia zebaki.

Viongozi wa vikundi vya wachimbaji wadogo kutoka mikoa ya Mwanza, Mara na Geita walishiriki ziara hiyo wakiongozwa na Baraza la udhibiti na usimamizi wa mazingira (NEMC) na timu ya wataalam kutoka Wizara ya Madini, Taasisi ya utafiti wa miamba na madini (GST) Dodoma na maafisa madini kutoka Mikoa ya kanda ya Ziwa na kutembelea maeneo ya uzalishaji wa dhahabu kwa kutumia njia mbadala.

Injinia John Shija kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) Dodoma, alishiriki ziara hiyo anafafanua kuwa matumizi ya zebaki ni njia pekee ya awali iliyotumika kuzalisha dhahabu duniani kote na kwamba bado nchi zinazoendelea zinatumia kemikali hiyo bila kujali madhara yake katika mazingira na afya ya binadamu.

 Alitoa mfano wa nchi ya Japan iliyozalisha dhahabu kwa wingi kutokana na kuwa na uchimbaji na matumizi makubwa ya zebaki na kusababisha watu wengi kupata madhara ya afya.

Kutokana na athari hizo utafiti ulifanyika kwenye machimbo ya Minemata, Japan na kubainika idadi kubwa ya wachimbaji na familia zao zimeathirika kiafya na kwamba matokeo ya utafiti huo ni chanzo cha ugunduzi wa njia mbalimbali za kuwakinga wachimbaji dhidi ya madhara yanayotokana na zebaki. 

Licha ya kubaini madhara makubwa, utafiti huo uliangalia pia namna wachimbaji wanavyoweza kujikinga kwa taratibu mbalimbali ili kuhakikisha hawaathiriki tena kwa zebaki.

Tanzania ambayo ni mwanachama wa mkataba wa Minemata, imeanzisha mradi wa miaka minne ulioanza Januari mwaka jana hadi Julai 2024 ambao unalenga kutekeleza mapendekezo ya mkataba huo unaotaka dunia kuondokana na matumizi ya zebaki katika uchenjuaji wa dhahabu.

Lengo ni kuanza maandalizi ya kukomesha matumizi ya zebaki na kwamba serikali isipofanya hivyo itabaki nyuma kwa sababu matumizi hayo yatakapofika mwisho wachimbaji wetu watakosa kemikali mbadala na kupunguza uzalishaji wa dhahabu unaoweza kuathiri pato la serikali na mchimbaji wenyewe

Injinia John Shija. 

Kwa upande wake Injinia Dr Befrina Igulu, msimamizi wa mradi wa udhibiti wa matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo kutoka Baraza la uhifadhi na usimamizi wa Mazingira (NEMC) anazungumzia hatua za Serikali kuanza kutekeleza mkataba wa Minemeta kwa lengo la kuridhia kwa vitendo utekelezaji wake na kupunguza matumizi ya zebaki duniani hasa kwa wachimbaji wadogo.

Kwa sasa tunakoelekea zebaki itakwisha na wachimbaji wadogo wenye matumizi makubwa watabaki nyuma wasipopewa njia mbadala,” anafafanua kuwa lengo kuu ni kuwezesha wachimbaji kuwa na matumizi sahihi bila kuathiri mazingira na afya na kwamba zebaki itaondolewa kuandaa teknolojia mbadala kabla ya kufika 2030.

Aidha, mradi huo unatekelezwa katika mikoa saba inayozalisha dhahabu ambayo ni pamoja na Mara, Mwanza, Geita, Shinyanga, Mbeya, Singida na Songwe.

Baraza la udhibiti na usimamizi wa mazingira (NEMC) ni mratibu wa mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano na wadau wake ikiwemo Wizara ya Afya, Tume ya madini, STAMICO, Mkemia mkuu wa Serikali, Taasisi ya Utafiti wa Miamba na Madini (GST), Vyuo vikuu na vyama au vikundi vya wachimbaji wadogo, wote wakiwajibika kumsaidia mchimbaji mdogo kufikia kuhama matumizi ya zebaki kwenda teknolojia mbadala isiyo na madhara kwenye mazingira na afya ya binadamu.

Kuhusu madhara ya zebaki Injinia Dr Befrina Igulu anakiri kuwa inaathiri binadamu na mazingira na afya ya binadamu

Dr Igulu ambaye ni msimamizi wa Mradi wa kupunguza athari na madhara ya zebaki kwa njia mbadala anasema

Madhara yake ni makubwa – kuzaa watoto wenye mtindio wa ubongo, midomo ya sungura, kudhoofika mwili, kutetemeka na kupoteza kumbukumbu. Inavuruga mfumo wa ubongo na kusababisha kudumaa kwa viungo vya mwili na ubongo

Wizara ya Afya na Mkemia mkuu wamepita kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini na kuchukuwa sampuli za damu, udongo, maji, samaki na viumbe wengine ambapo taarifa yao inasubiriwa kuelezea ukubwa wa madhara na maelekezo ya hatua za kufanya.

Tunasubiri matokeo ya tathimini ya Wizara ya Afya hapa kwetu inayoendelea kufanya tafiti zake, na inaonyesha idadi kubwa ya watoto na wanawake hasa wenye uwezo na umri wa kubeba mimba wameathirika zaidi hasa wanaoishi katika maeneo ya migodini. 

Dr Befrina Igulu

Aidha anatoa wito kwa wachimbaji wote kupata elimu ya kutosha juu ya madhara ya zebaki na kuchukuwa hatua kwani madhara hayo hayabaki kwa wachimbaji husafiri hadi kwa jamii na kuenea kwenye mazingira.

Njia pekee ni kupunguza matumizi ya zebaki kwa wachimbaji wadogo, kuwasaidia kuakutafuta na kuhamia kwenye teknolojia mbadala bila kuangalia gharama kwani wakiungana ni rahisi kufikia lengo la kusimika mitambo mikubwa yenye uwezo wa kuongeza uzalishaji wa dhahabu na kuondokana na madhara ya zebaki katika mazingira na afya ya binadamu.

Edica Masisi ni Meneja Maeneo maalum na Mabadiliko ya Tabia nchi kutoka NEMC, anafafanua kuhusu ziara ya kujifunza kwa wachimbaji na kuona matumizi ya njia mbadala yanayofanya wachimbaji wanafanya kazi kwa kujiamini bila hofu ya kuvunjika mbao, kuwaangukia na kuwafukia. Wachimbaji wanawasiliana kwa simu maalum ya umeme na kujiokoa mapema wanapopata hitilafu.

Baada ya kukamilisha ziara hiyo ya mafunzo, mchimbaji mmoja mdogo wa eneo la Nyakagwe, Endrew Karama, anamwaga shukrani kwa Baraza la udhibiti na usimamizi wa mazingira (NEMC) kwa kuita baadhi ya wachimbaji kushuhudia madhara ya zebaki na kuona mbinu mbadala ya uchimbaji na uchenjuaji wa dhehabu.

Karama ambaye ni kiongozi wa GERAMA, Taasisi inayoshughulikia wachimbaji wadogo Mkoa wa Geita anasema

Tumejifunza njia mbadala na matumizi ya mitambo isiyotumia zebaki

Flora Rashid pia ni mchimbaji mdogo kutoka Mkoa wa Mara, amesema mtu aliyeathirika kwa zebaki hana tofauti na mtu mwenye HIV na kwa upande wa mtoto alimfahamu mama aliyekuwa anapembua mawe ya dhahabu na kutumia zebaki kunasa dhahabu wakati akiwa mjamzito hadi alipojifungua lakini mtoto alidumaa na kuonekana mdogo kwa wenzake aliowazidi umri.  Anatoa wito kwa wanawake wajawazito na watoto wasifanye kazi za migodini na kwamba wanawake wanaofanya hivyo wakiwa na watoto wanahatarisha afya zao na watoto kwani vumbi la mgodi lina chembechembe za madini hatari kwa watoto.

Mbaraka Yahaya, Meneja Idara ya Maabara na uzalishaji dhahabu kwenye mgodi binafsi wa Kadeo Christopher, unaotumia mfumo wa zebaki, kwa kuchakata kwenye kigida cha kuzalisha dhahabu

Mgodi wetu unampango wa kuanzisha mpango wa kutumia CIP ili kuzalisha zaidi ifikapo mwaka 2023.

David Peter, mchimbaji wa Irasamilo, Buhemba wilaya ya Butiama na kiongozi wa wachimbaji wadogo kupitia chama cha wachimbaji mkoa wa Mara.  Amejifunza uwezekano kwa wachimbaji wadogo kuachana na mfumo hatari wa kutumia zebaki na kupongeza STAMICO kwa kuja na kituo cha mfano. 

Uwezekano wa kujenga kituo mikononi mwetu mmoja mmoja au kwa kujiunga. Nimebaini kuwa upatikanaji wa dhahabu ni mkubwa lakini njia ya zamani ilikuwa inapoteza mapato, muda wa uzalishaji dhahabu na kwa mtambo mpya tutavuna zaidi

Peter.

 

 

 

Post a Comment

0 Comments