DK.MPANGO AAGIZA STAMICO,NEMC,NA WIZARA YA MADINI KUONGEZA KASI UKAGUZI MAENEO YA UCHIMBAJI MADINI.

 ðŸ“ŒRHODA SIMBA

MAKAMU wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameagiza Wizara ya Madini, STAMICO na NEMC kuongeza kasi ya ukaguzi maeneo ya uchimbaji madini katika kuzingatia uhifadhi wa mazingira.

Dkt.Mpango ametoa maagiza hayo leo Agosti 12,2022 jijini Dodoma katika hafla ya kutimiza miaka 50 ya shirika la Madini la Taifa [STAMICO] iliyokwenda sambamba na kaulimbiu isemayo “Tunajivunia kutimiza miaka 50 kwa kishindo.

Dkt.Mpango ametoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya maeneo mengi ya uchimbaji wa madini kutozingatia uhifadhi wa mazingira hali ambayo husababisha watu wanaozungukwa na migodi kuvuta vumbi na kusababisha magonjwa na kugharimu maisha ya watu.

Hivyo ameagiza Wizara ya madini kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri mkuu kuweka kipaumbele cha utunzaji wa mazingira na kutoa elimu kwa wachimbaji madini namna ya kujikinga na vumbi mahala pa kazi.

Aidha, ametoa rai kwa taasisi za fedha kutoa mikopo yenye masharti nafuu ili wachimbaji wadogo waweze kupata fursa ya kupata mikopo na kuweza kupata vifaa vya kisasa vya uchimbaji madini huku akiitaka STAMICO kushirikiana na SIDO namna ya kutengeneza vifaa vyenye gharama nafuu.

Kuhusu ajira za watoto migodini Dkt.Mpango ameagiza taasisi zinazohusika ziendee kukomesha suala hilo ili kulinda afya za watoto.

Waziri wa Madini Dkt.Doto Biteko amesema shirika la Madini la Taifa [STAMICO] limekuwa na mchango mkubwa katika kufufua maeneo ya uchimbaji madini yaliyofifia kutokana na kuacha kuendelezwa huku Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt.Seleman Jafo akisema Wizara yake imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha sekta ya uchimbaji madini inakuwa rafiki katika utunzaji wa mazingira.

Makamu Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Seif Gulamali amesema kamati hiyo imekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inatengwa bajeti ya kujitosheleza katika sekta ya madini.

Aidha, amesema STAMICO imefanya Mapinduzi makubwa kwa kuzalisha Tsh.Bilioni 48 na kutumia fursa hiyo kulipongeza shirika hilo kwani hiyo itasaidia kuacha utegemezi na kujisimamia yenyewe na kupongeza kwa kuja na mpango wa mkaa mbadala katika utunzaji wa mazingira.

Akitoa historia fupi ya shirika hilo, Makamu mwenyekiti shirika la madini la Taifa [STAMICO] Dkt.Venance Mwase amesema Agosti 1972 busara ilitumika kuanzisha shirika hilo kwa lengo la uvunaji rasilimali madini kwa niaba ya umma katika kuwekeza mnyororo mzima wa madini ikiwemo uchenjuaji, uwekaji thamani hadi hatua ya mwisho.


Pia amesema dhumuni jingine la shirika la Madini la Taifa ni kumwezesha mchimbaji mdogo kushiriki katika uchimbaji wa madini ikilinganishwa na mashirika mengine.

Malengo ya serikali ni kuhakikisha sekta ya madini inachangia pato la taifa dola bilioni 5.5 kwa mwaka huku STAMICO ikiongeza mapato kutoka Tsh.Bilioni 1.6 hadi bilioni 40 ambapo pia leo imetoa gawio la Tsh.Bilioni 2.2 kwa serikali.


 

Post a Comment

0 Comments