SHIRIKA
la Foundation for Civil Society (FCS) limetoa ruzuku ya Shilingi 3,957,301,580 ambazo
ni sawa na Bilioni nne (4) kwa asasi za kiraia (AZAKI) 89 Tanzania bara na
visiwani ili kutekeleza miradi ya kimaendeleo chini ya programu za utawala bora
katika sekta za asasi za kiraia.
Akizungumza
katika warsha ya usimamizi wa ruzuku kwa AZAKI hizo zilizochaguliwa kupata
ruzuku jijini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Francis Kiwanga amesema FCS
imejikita katika kuhakikisha miradi inayofadhiliwa inawasaidia wananchi katika
kuboresha maisha yao na kukuza sekta za asasi hizo.
Amesema
miongoni mwa sekta hizo ni pamoja na sekta ya maji, elimu, afya na kilimo;
usawa wa kijinsia; ujumuishwaji wa vijana na watu wenye ulemavu, na ujenzi wa
amani na mshikamamo wa kijamii kwa mwaka 2022/2023.
FCS imepitisha mpango mkakati mpya wa mwaka 2022-2026 ambao unataka kuona wananchi waliowezeshwa, wastahimilivu, wanaowajibika na wanaopata haki za kiuchumi, kijamii na kuboresha ubora wa maisha yao.
Aidha Meneja wa miradi foundation civil society (FCS) Edna Chilimo amesema ili kuwafikia wananchi ni muhimu kufanya kazi na asasi za kijiji, kata na wilayani pamoja na wabia wa mashirika yanayofadhiliwa katika kuleta mabadiliko na maendeleo.
Tunajengea uwezo Azaki ili kuweza kuandaa na kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwemo Serikali, Sekta binafsi, Mwananchi na Azaki nyingine na tumekuwa walezi wa sekta ya AZAKI
FCS
ni shirika huru la maendeleo, la Kitanzania lisilolenga kupata faida, ambalo
hutoa ruzuku na huduma za kuzijengea uwezo asasi za kiraia nchini Tanzania na
limechangia kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha uwezo wa sekta ya kiraia
nchini Tanzania.
0 Comments